Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Thomas Laban amekemea matumizi mabaya ya fedha za umma kuagiza kuchukuliwa hatua kwa watumishi wanaohujumu mapato ya serikali.
Kanali Laban ametoa agizo hilo wakati anazungumza na watumishi wa umma wakiwemo madiwani wa Wilaya ya Mbinga katika ziara ya kikazi ya kujitambulisha rasmi kwa watumishi baada ya kuteuliwa na Rais kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Agosti mwaka huu.
“Sitakuwa na masihara na mtu yeyote anayecheza na makusanyo ya fedha za umma kupitia POS ,matumizi mabaya ya fedha za umma ikiwemo kufanya ziara za mafunzo nje ya Mkoa ambazo hazina tija ni matumizi mabaya ya fedha za umma,sitaruhusu vibali vya ziara hizo’’,alisisitiza Kanali Thomas.
Mkuu wa Mkoa pia ameagiza kushughulikia maslahi ya watumishi wa umma kwa wakati na kuimarisha mahusiano mazuri kati ya watumishi wa chini na wakuu wa ili kuongeza ari na utendaji kazi.
Ametoa rai kwa watumishi wa umma kujiandaa na kusitaafu ambapo amewataka watumishi hao kutambua kuwa siku wanayoajiriwa ndiyo siku ambayo wanatakiwa kuanza kujiandaa kustaafu.
RC Thomas amewaagiza maafisa Ugani kusimamia zoezi la kusajiri wakulima kwa ajili ya zoezi la mbolea ya ruzuku Pamoja na kusimamia kilimo cha Pamoja huku akisisitiza usafi wa mazingira na upandaji wa miti kufanywa na kila kaya ili kutunza mazingira.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amewaagiza madiwani kuhakikisha wanasimamia miradi yote inayotekelezwa katika Kata zao na kusisitiza kuwa sio sifa kuwa na miradi ambayo haikamiliki.
Awali akizungumza kwenye kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mheshimiwa Aziza Mangasongo amesema watumish 176 wamepandishwa vyeo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ambapo serikali imelipa zaidi ya shilingi milioni 440 za malimbikizo ya mishahara kwa watumishi.
Amesema licha ya Halmashauri hiyo kuwa na watumishi 2015 ,bado inakabiliwa na upungfu mkubwa wa matumishi katika kada za elimu,afya na maendeleo ya jamii.
Amezitaja changamoto kubwa zinazowakabili watumishi katika wilaya hiyo kuwa ni mikopo umiza, madeni mengi kwa watumishi na baadhi ya watumishi wanaokaribia kustaafu kutapelewa hali ambayo inapunguza ari ya utendaji kazi kwa watumishi.
Akizungumzia utekelezaji wa kilimo cha Pamoja,Mheshimiwa Mangasongo amesema wilaya imeandaa hekari 2000 katika Kijiji cha Matiri na hekari 123 katika Kijiji cha Ruanda kwa ajili ya utekelezaji wa kilimo cha Pamoja.
Wilaya ya Mbinga ni moja kati ya wilaya tano za Mkoa wa Ruvuma yenye vitongoji 780 na vijiji 117.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ruvuma
Septemba 21,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.