Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kuongeza juhudi katika kushughulikia hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), licha ya halmashauri hiyo kupata hati safi.
Akizungumza kwenye Baraza Maalum la kujadili hoja za CAG kwa mwaka 2023/24, ambalo limefanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo, Kanali Ahmed amesisitiza umuhimu wa kuongeza kasi katika utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na CAG.
"Nimesikia hapa kulikuwa na hoja na mapendekezo 27 yaliyotolewa na CAG, kati ya hayo yaliyofanyiwa kazi na kufungwa ni saba, yanayoendelea na utekelezaji ni 20, ukiangalia hapa kasi ya ushughulikiaji na ufungaji wa hoja ni ya kusuasua, mnahitajika kuongeza kasi," alisema Kanali Ahmed.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Phiniel Mbula, amesema kuwa wanatoa vyeti kwa watumishi waliosaidia upatikanaji wa hati safi katika halmashauri lengo likiwa ni kutambua mchango wao mkubwa katika kufunga hesabu kwa kuzingatia viwango vya kihasibu vya kimataifa, sheria, na kanuni za fedha.
Ameongeza kuwa upatikanaji wa hati safi ni matokeo ya weledi, uadilifu, na uzalendo uliooneshwa na mkurugenzi, madiwani na kushirikiana na sekretarieti ya mkoa.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Namtumbo, Fransis Mgoloka, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, ameipongeza halmashauri hiyo kwa mafanikio hayo, huku akiahidi kuendelea kufuatilia na kufanyia kazi hoja zilizobaki ili ziweze kupatiwa majibu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.