Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amewapongeza wasimamizi wa mradi wa ujenzi wa hospitali ya Manispaa ya Songea iliyopo eneo la Sanangula, Kata ya Shule ya Tanga.
Ametoa pongezi hizo alipotembelea na kukagua maendeleo ya Hospitali hiyo ambapo amesisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya ujenzi na kuhakikisha kazi zinamalizika kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma za afya katika eneo la karibu.
"Nimekuja kuona utekelezaji wa miradi ndani ya Mkoa wetu wa Ruvuma ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kwamba ikifika Disemba miradi mingi iliyopatiwa fedha iwe imekamilika," alisema Kanali Abbas
Amewataka watumishi wa hospitali hiyo kutoa huduma zinazolingana na taaluma yao kama wahudumu wa afya ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Amesisitiza kuwa mtaalam wa afya anatakiwa kuwa na huruma, kutoa huduma bora kwa wagonjwa na mwenye kujali, hivyo amewataka kuyazingatia hayo ili wananchi wanapoenda kupata huduma waone wapo kwenye eneo salama na sio eneo la manyanyaso.
Naye Mganga Mkuu wa Manispaa ya Songea Dr. Amos Mwenda amesema mradi huo ulianza kutekelezwa tarehe 9 Disemba 2021 na hadi kufikia Septemba 2024 Halmashauri ya Manispaa ya Songea imepokea Shiningi Bilioni 1.1 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo.
Ameongeza kuwa mradi huo uliibuliwa na wananchi wa kata ya Shule ya Tanga kupitia mpango wa fursa na vikwazo ili kupunguza kero na umbali wa upatikanaji wa huduma za afya.
Awali wananchi wa kata ya Shule ya Tanga walilazimika kutembea kwa umbali wa kilometa 20 kufuata huduma za afya katika kituo cha afya cha Mjimwema na hospitali ya Rufaa ya Mkoa ,Songea
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.