MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amezindua usajili wa wamachinga kwa njia ya vocha katika eneo la soko la Majengo Manispaa ya Songea.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo uliowashirikisha viongozi na wanachama wote wa Shirikisho la Wamachinga Mkoani Ruvuma,Kanali Thomas amesema uzinduzi wa usajili wa Wamachinga ni mafanikio makubwa kwa Wamachinga yaliyopatikana katika serikali ya Awamu ya Sita.
“Kupitia usajili huu serikali itaweza kuwa na taarifa sahihi za wanachama wa Shirikisho la Umoja wa Mchinga (SHIUMA) kwa nchi nzima na kuwezesha kuweka mipango yake vizuri katika kusaidia kukuza sekta hii muhimu ya wajasirimali wadogo’’,alisisitiza.
Amesema kwa muda mrefu Wamachinga walikuwa wanafanya shughuli zao kwa usumbufu ambapo hivi sasa baada ya kutambuliwa,serikali imeweza kufanikisha kuanzisha umoja wa SHIUMA na kwamba hivi sasa kila Halmashauri ndani ya Mkoa wa Ruvuma kuna uongozi ambao unashirikina na Mamlaka za serikali kusikiliza na kutatua changamoto za Wamachinga.
Ametoa rai kwa Wamachinga kuhakikisha vitambulisho vilivyotolewa na serikali wanavitumia vizuri kwa ajili ya shughuli zao ambapo amesema vitambulisho hivyo pia vinaweza kuwasaidia katika maswala mbalimbali ya kuwatambua.
Amesisitiza kuwa Mjasirimali mdogo akisajiliwa kwa njia ya mtandao atatambulika rasmi na viongozi Pamoja na wadau hivyo kuweza kukuza sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya Uchumi na uwezeshaji wananchi.
Hata hivyo amesema zoezi la utoaji vitambulisho lilisimama kwa muda na sasa serikali inaandaa utaratibu mzuri zaidi kwa kushiriakina na Wizara ya Maendeleo ya Jamii ili kuboresha vitambulisho vya Wamachinga.
Amesema Mkoa umetenga maeneo rasmi waliyopangiwa Wamachinga kufanya shughuli zao na kwamba serikali itaendelea kuboresha miundombonu na mazingira wezeshi ili kutoa huduma bora.
Kanali Thomas amesema serikali imewezesha kupatikana mikopo kwa riba nafuu kupitia benki ya NMB kwa ajili ya Wamachinga na kwamba matarajio ya serikali baada ya miaka kadhaa Wamachinga wawe wafanyabiashara wakubwa .
Kwa upande wake Mwenyekiti wa SHIUMA Mkoa wa Ruvuma Salum Masamaki ameipongeza serikali kwa kutatua kero mbalimbali zinazowakabili ikiwemo suala la kupata mikopo ambapo amesema hivi sasa Wamachinga kutoka Manispaa ya Songea wameanza kunufaika na mikopo kutoka benki ya NMB,
Amesema mikopo hiyo inawawezesha wajasirimali hao wadogo kukuza na kuendeleza biashara zao na kwamba baada ya kujisajiri wataweza kutambulika na Taasisi za fedha hivyo kupata mikopo na elimu mbalimbali za fedha.
Masamaki amesisitiza kuwa usajiri huo utawawezesha kupata kitambulisho cha Shirikisho la Umoja wa Wamachinga hivyo kuweza kupata huduma zote zinazotolewa na Shirikisho.
Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akiwa na Mwenyekiti wa SHIUMA Mkoa wa Ruvuma Salum Masamaki kwenye uzinduzi wa usajili wa usajili wa Wamachinga kwa njia ya vocha eneo la Majengo Manispaa ya Songea
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.