Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amewaagiza wakuu wa Idara katika Halmashauri kushiriki ipasavyo katika kuandaa majibu ya hoja na utekelezaji wa mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kanali Abbas ametoa maagizo hayo kwa nyakati tofauti wakati anazungumza katika kikao cha kujadili utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 katika Halmashauri za Nyasa,Mbinga Mji na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
Mkuu wa Mkoa ametoa maagizo hayo baada ya kutoridhishwa na utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya LAAC kwenye Halmashauri hizo.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Kamati ya Bunge ya LAAC Agosti 2023 ilitoa maagizo manne ambapo hadi sasa hakuna agizo hata moja lililotekelezwa,katika Halmashauri ya Nyasa LAAC ilitoa maagizo kumi ambapo kati ya maagizo hayo hadi sasa ni maagizo mawili tu yametekelezwa na katika Halmashauri ya Mbinga Mji kati ya maagizo Matano yaliyotolewa hakuna agizo hata moja lililotekelezwa.
“Hali ya utekelezaji wa maagizo ya LAAC hairidhishi kabisa,katika Halmashauri za Mbinga Mji na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga hakuna hata agizo moja ambalo limetekelezwa na kufungwa hadi sasa,kwanini maagizo hayo yote bado hayajafungwa?’’,alihoji RC Abbas.
Kanali Abbas pia ameelezea mwenendo wa ushughulikiaji wa Hoja na mapendekezo ya CAG katika Halmashauri hizo tatu bado hauridhishi ambapo amewaomba waheshimiwa madiwani kufuatilia kwa karibu na kuhakikisha hoja zinajibiwa ipasavyo na kuhakikisha kuwa hoja hizo hazijirudii tena.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa ameiagiza Sekretarieti ya Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na Menejimenti ya Halmashauri kupitia majibu na vielelezo vyote kabla ya kuwasilisha kwa CAG kwa ajili ya uhakiki.
Mkuu wa Mkoa pia ameziagiza Halmashauri hizo kuchukua hatua mapema za kinidhamu kwa watumishi wanazozalisha hoja .
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Rehema Sefu Madenge akizungumza kwenye kikao hicho amesema hoja zote zilizoagizwa na LAAC zimetokana na utekelezaji wa shughuli kwenye Halmashauri husika hivyo Halmashauri zinahusika moja kwa moja kujibu hoja hizo.
Amesisitiza kuwa hoja hizo zilizoibuliwa zina majibu hivyo amewaagiza watendaji hao kuhakikisha wanajibu hoja zote ili zifungwe na kuweka mkakati thabiti wa kuhakikisha hoja hizo hazijitokezi tena.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbinga Mheshimiwa Deusderius Haule ameamhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kuwa atasimamia kikamilifu kuhakikisha wanatekeleza maagizo ya kujibu hoja za LAAC na kutekeleza mapendekezo ya CAG.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Rehemu Sefu ,Madenge akizungumza kwenye kikao cha mapitio ya utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Hesabu za Serikali za Mitaa Halmashauri ya Nyasa
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.