RC RUVUMA AZINDUA MIONGOZO MITATU YA ELIMU
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amezindua miongozo mitatu ya usimamizi na uendeshaji wa elimu.
Hafla ya uzinduzi huo imehudhuriwa na wadau wa elimu kutoka wilaya zote tano za Mkoa wa Ruvuma na kufanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari ya Songea Girls mjini Songea.
Akizungumza kabla ya kuzindua miongozo hiyo Kanali Thomas amewaagiza wasimamizi wa elimu kusimamia na kuondoa changamoto ya baadhi ya wanafunzi kutomudu stadi za Kuandika, Kuhesabu na Kusoma (KKK).
“Mkaondoe udhaifu wa baadhi ya viongozi katika usimamizi na ufuatiliaji,kasimamieni na kuweka mikakati ya kupunguza au kuondoa kabisa uhaba wa miundombinu ya shule hasa vyoo vya wanafunzi’’,alisema RC Thomas.
Mkuu wa Mkoa amewaagiza wadau wote wa elimu kuondoa utoro wa baadhi ya wanafunzi na walimu.
Hata hivyo amesema miongozo hiyo imechambua changamoto mahususi katika elimu ya awali,msingi na sekondari na kwamba mikakati ya muda mfupi na mrefu ya utatuzi wa changamoto imebainishwa katika miongozo hiyo.
Awali Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Jeremiah Sendoro aliitaja miongozo mitatu ambayo imezinduliwa kuwa ni Mwongozo ambao umeainisha changamoto katika elimu ya msingi na sekondari.
Ameutaja mwongozo wa pili kuwa unahusu mkakati wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji katika ngazi ya elimu ya msingi na mwongozo wa tatu umeeleza kuhusu uteuzi wa viongozi wa elimu katika mamlaka za serikali za mitaa na mikoa.
Hata hivyo amesema miongozo yote mitatu imebeba changamoto na taratibu za usimamizi na uendeshaji wa elimu ya msingi na sekondari na kwamba miongozo hiyo inakusudia kuleta tija katika sekta ya elimu kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Naye Afisa Elimu Mkoa wa Ruvuma Emanuel Kisongo amesema miongozo hiyo inatarajia kuwa ni muarubaini wa changamoto za elimu hapa nchini.
Kisongo amesisitiza kuwa miongozo hiyo imebeba zana ya kurudi darasani na kuwapa wanafunzi kile kinachostahili na kwamba wadau wote wa elimu wanatakiwa kusimamia kikamilifu utoaji elimu.
Miongozo hiyo mitatu imeundwa Julai mwaka huu kupitia Wizara ya TAMISEMI ikiwa ni juhudi za serikali ya awamu ya sita kuboresha elimu ili wananchi wake wapate elimu bora na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Tanzania.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ruvuma
Septemba 10,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.