REDCROSS Ruvuma ilivyohamasisha uchangiaji damu chupa 800
MRATIBU wa Damu Salama katika Mkoa wa Ruvuma Imani Mbuzi amelipongeza Shirika la Msalaba Mwekundu(Red cross) Tanzania Mkoa wa Ruvuma kwa kuhamasisha uchangiaji damu chupa 800.
Mbuzi ametoa pongezi hizo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma ambayo siku ya kilele cha maadhimisho ya uchangiaji wa damu kitaifa ambayo yalianza Juni tano hadi Juni 14 mwaka huu.
“Shabaha ilikuwa ni kila Halmashauri kuchangia chupa 100 za damu na kufanya jumla ya chupa 800 katika Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma,kutokana na uhamasishaji mkubwa unaofanywa na Redcross tutavuka lengo kwa sababu idadi ya watu wanaojitokeza ni kubwa’’,alisisitiza Mbuzi.
Amesema katika kituo cha hospitali ya Rufaa ya Mkoa hadi sasa zimekusanywa uniti zaidi ya 55 na kwamba idadi ya watu wanaojitokeza kuchangia damu imeongezeka kutoka watu wawili kwa siku hadi 12 kwa siku na kwamba hali hiyo imetokana na uhamasishaji mkubwa unaofanywa na Redcross Mkoa wa Ruvuma.
Amesema Redcross wamefanyakazi kubwa ya kwenda kwenye mikusanyiko ya watu kama sokoni,nyumba za ibada, madereva wa pikipiki,barabarani na kuhamasisha kuchangia damu hali ambayo imesababisha wengi kujitokeza.
Amesema bila Redcross uchangiaji wa damu mwaka huu ungekuwa na changamoto kubwa kutokana na janga la corona ambalo limesababisha kushindwa kuweka mahema sehemu za wazi na kutangaza ili watu wafike kuchangia.
Mwenyekiti wa Redcross Mkoa wa Ruvuma Judith Kapinga amesema wateja wote ambao wamehamasishwa katika maeneo mbalimbali hivi sasa wanafika kwenye vituo vya kuchangia damu.
Amesema mwitikio wa watu ni mkubwa licha ya kukabiliwa na changamoto za kuacha shughuli zao kwa muda na kufika kuchangia damu vituoni na kwamba Redcross imedhamiria kuvuka malengo ya uchangiaji damu ili kuwa na benki ya kutosha ya damu na kuokoa maisha ya watanzania wanaohitaji damu.
“Wahitaji wa damu ni wengi wakiwemo mama wajawazito,watoto chini ya miaka mitano,watu waliopata ajali,watu waliozaliwa na seli nundu na watu wanaofanyiwa upasuaji,hawa wote ni wahanga wa damu’’,alisisitiza.
Deredia Hamuya ni Mhamasishaji wa uchangiaji wa damu kutoka Redcross Mkoa wa Ruvuma,amesema Redcross imeshiriki kikamilifu kuhamasisha katika Halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma ili wajitokeze watu wengi kuchangia damu na kuokoa maisha.
“Baada ya kuhamasishwa wengi wamejitokeza,wameelewa nini maana ya uchangiaji damu,suala la uchangiaji damu ni la kila mtanzania,thamani ya damu hailinganishwi na kitu chochote changia damu okoa maisha’’,alisema.
Zoezi la uhamasishaji wa uchangiaji damu linafanyika nchini kote kila baada ya miezi mitatu ambapo linatarajiwa kufanyika tena Septemba mwaka huu.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Juni 14,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.