KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Joseph Konyo amewataka madereva wote kufuata sheria na kanuni za barabarani ili kuepuka ajali zisizo za lazima.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Songea Club Manispaa ya Songea.
Akizungumza katika kikao hicho Kamanda Konyo amesema kuna changamoto chache ambazo zinaleta mtazamo hasi kati ya jeshi la Polisi na madereva hivyo amesisitiza wafuate sheria na taratibu zote kama kuvaa kofia ngumu, kuwa na leseni, kuendesha mwendo mzuri na kupaki sehemu sahihi ili kuepuka migogoro na Jeshi la Polisi.
‘’Naungana mkono wa dhati kabisa na waliosema kazi ya bodaboda na bajaji ni kazi sawa na kazi nyingine, na kazi ya Jeshi la Polisi ni kulinda raia na mali zao na madereva wa bajaji na bodaboda wana mali zao lazima tuwalinde’’, amesema RPC Konyo.
Aidha, RPC Konyo amesema mwaka 2020 kuanzia Januari hadi Desemba ajali za pikipiki zilikuwa 16 watu waliofariki kwenye ajali hizo walikuwa 22 majeruhi 13 na pikipiki zilizoathirika na ajali zilikuwa 26, na kwamba kwa mwaka 2021 ajali zilikuwa saba, watu waliokufa wanne, majeruhi sita na pikipiki 12 zilizoathirika na ajali hiyo.
RPC konyo ametoa rai kwa madereva wote kwa ujumla kujitokeza kushiriki Sensa ya Watu na Makazi ambayo inatarajia kufanyika Agosti 2022.
Kwa upande wake Kamnada wa Usalama Barabarani Mkoa wa Ruvuma RTO Salum Morimori amelitaja tatizo kubwa ambalo lipo kwa madereva wa bodaboda na bajaji ni kutokuwa na utayari wa kuhudhuria mafunzo ya udereva na kupata leseni, hivyo amewashauri madereva hao kutumia Elimu waliyoipata darasani na kufuata sheria zote za barabarani ili kupunguza ajali.
Naye Katibu wa Umoja wa Madereva Bajaji Songea Albert Nchimbi ameomba madereva waelekezwe , waonywe na wapewe Elimu juu ya makosa wanayoyafanya kabla ya kuandikiwa faini na kuwekwa mahabusu.
Imeandikwa na Bahati Nyoni
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Machi 24 2022.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.