Na Albano Midelo
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed ameipongeza serikali kupitia Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kwa kuuwezesha Mkoa kuwa kituo cha pili kwa ukubwa hapa nchini kwa uzalishaji wa mbegu bora.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya mkulima yaliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya shamba la mbegu Namtumbo linalomilikiwa na ASA,Kanali Abbas amelitaja shamba hilo la kuzalisha mbegu kuwa ni la pili kwa kubwa nchini likiwa na hekta 3,580.4.
“Hii ni fursa kubwa kwetu tulioendelea kupewa na Taifa,licha ya Mkoa wa Ruvuma kuwa wazalishaji wa kwanza nchini wa mazao ya chakula na nafaka ,bado Mkoa umeendelea kupata heshima ya kuwa ni kituo cha uzalishaji mbegu wa mbegu bora cha pili kwa ukubwa ndani ya Taifa letu’’,alisisitiza Kanali Abbas.
Ameipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuamua kulirudisha shamba la NAFCO Namtumbo kuwa miongoni mwa mashamba ya serikali yanayozalisha mbegu bora ambazo zitaongeza uzalishaji mazao ya chakula na serikali kujihakikishia usalama wa chakula.
Ameongeza kuwa mbegu bora zinazozalishwa kwenye kituo hicho zitapatikana kwa gharama nafuu na kwamba mradi huo umetoa fursa kwa wawekezaji wa kilimo cha mkataba ambapo ameiagiza ASA kuhakikisha wanapatikana wawekezaji wengi wa mkataba ili shamba hilo lisibaki kuwa mapori.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ametoa rai kwa ASA kuhakikisha wanafanya kilimo cha kisasa kwa kuondokana na kilimo cha matumizi ya vifaa duni badala yake kuongeza kasi ya kutumia vifaa vya kisasa.
Hata hivyo amesema licha Mkoa kufanya vizuri kwenye kilimo,bado Mkoa unaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe na kuwepo vivutio vikubwa vya utalii vinavyoupambanua Mkoa .
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) Dkt.Sophia Kashenge akizungumza kwenye maadhimisho hayo amelitaja shamba la mbegu Namtumbo lenye ukubwa wa hekta 3,580.4 kuwa ni miongoni mwa mashamba 16 ya mbegu yenye jumla ya hekta 17,710.26.
Ameyataja mashamba hayo ya mbegu yanapatikana katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Ruvuma, Tanga, Pwani, Arusha, Tabora, Kigoma,Katavi na Geita na kwamba shamba la mbegu Namtumbo ni la pili kwa ukubwa hapa nchini likiwa na watumishi 15.
Amesema katika msimu wa mwaka 2023/2024,shamba la mbegu Namtumbo linatarajia kuzalisha mbegu Zaidi ya tani 1,275 za mazao mbalimbali yakiwemo mahindi na alizeti .
Amelitaja shamba la mbegu Namtumbo kuwa limetoa mchango mkubwa wa kukabiliana na upungufu wa chakula katika mikoa mingine ikiwemo wilaya ya Nzega Mkoa wa Tabora na Wilaya ya Hanang Mkoa wa Manyara .
Kulingana na Dkt. Kashenge, mikakati ya shamba hilo ni kuongeza uzalishaji wa mbegu za mafuta hasa alizeti na ufuta ili kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula na kupuguza uagizaji wa mafuta toka nje ya nchi hali ambayo itapunguza matumizi ya fedha za serikali katika kuagiza mafuta hayo nje.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mheshimiwa Ngollo Malenya ameitaja Wilaya hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuufanya Mkoa wa Ruvuma kuwa ghala la chakula nchini ambapo katika msimu uliopita wilaya ilizalishaji mahindi Zaidi ya tani 1,552,955 na kwamba msimu huu Wilaya inatarajia kuzalisha mahindi Zaidi ya tani 1,920,550.
Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) ulianzishwa chini ya sheria ya Wakala za Serikali namba 30 ya mwaka 1997 lengo kuu likiwa ni kuongeza uzalishaji na upatinaji wa mbegu bora kwa wakulima kwa bei nafuu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.