Ruvuma Kuimarisha Mapambano Dhidi Ya UKIMWI-RC Mndeme
Tunduru.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amezitaka taasisi na wadau wa mapambano dhidi ya UKIMWI kuongeza jitahada za kuzuia maambukizi mapya kuongezeka.
Ametoa agizo hilo Leo (Jumamosi tarehe 01.Desemba,2018) katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika kimkoa katika uwanja wa Baraza la Idd wilaya ya Tunduru.
Akitoa hotuba kwa niaba ya Mkuu huyo wa Mkoa,Mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma Homera amesema takwimu zinaonyesha Ruvuma ina kiwango cha maambukizi ya VVU/UKIMWI cha asilimia 5.6 zaidi ya kile cha Taifa cha asilimia 4.7 kwa mwaka 2016/2017.
Takwimu hizi ingawa zinaonekana kushuka kwa kiwango cha maambukizi kutoka asilimia 7 mwaka 2011/2012 bado kunahitajika nguvu na mikakati mipya ya kushusha zaidi kiwango cha maambukizi ya VVU.
Ili kuhakikisha maambukizi mapya yanapungua Mndeme amesisitiza mkakati wa upimaji wa hiari wa VVU uimarishwe kwenye wilaya zote tano.
Ameongeza kusema ni wakati sasa kuhakikisha watu wote wanaokutwa na VVU wanaanzishiwa tiba mara moja.
Mkuu wa wilaya Homera ameishukuru serikali ya awamu ya Tano kwa kuongeza bajeti ya dawa hadi kufikia Shilingi Bilioni1.3 kwa mkoa wa Ruvuma kufikia mwezi Juni 2018 ikilinganishwa na shilingi milioni 297.5 zilizotolewa mwaka 2016/2017 kwenda Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Mafanikio haya amesema yamesaidia wananchi wengi wa mkoa wa Ruvuma kuwa na uhakika wa matibabu hivyo kuongeza jitihada za kupunguza kasi ya maambukizi ya VVU.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt.Magdalena Zenda amesema katika kipindi cha Januari hadi Octoba 2018 jumla ya wananchi 456,777 walipimwa hali zao za maambukizi.
Kati yao waliogundulika na maambukizi ni 8,494 ambapo wanaume walikuwa (3,764) na wanawake (4,730).
Dkt .Zenda ameongeza kusema hadi kufikia mwezi Octoba 2018 Mkoa umefanikiwa kusajili na kuanzisha dawa za kufubaza Virusi (ARV) kwa WAVIU 63,671 tangu huduma hizi zianze mwaka 2004.
"Kati yao wanaotumia dawa hadi sasa ni 42,056 ,wanaume ni (14,336) na wanawake (27,720) wanaendelea kupata huduma katika kliniki za tiba na matunzo (CTC) kote mkoani " alisema Dkt.Zenda.
Ametaja changamoto kubwa ni idadi ya wanaotumia ARV wapatao 14,899 kuhamia vituo vingine nje ya mkoa na 11,368 ni waVVU waliopoteza ufuasi.
Katika kipindi cha mwaka 2004 hadi sasa mkoa umekuwa na vifo vitokanavyo na UKIMWI 7,168 .
Mkoa wa Ruvuma wenye watu takribani 1,449,830 kwa sensa ya mwaka 2012 una vituo vya kutolea huduma za afya 314.
Kati yake hospitali zipo (11),vituo vya afya (32) na zahanati (271) hii inafanya huduma za upimaji na matibabu ya VVU kupatikana karibu maeneo yote.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI mwaka huu 2018 inasema " Know your status" -Pima,Jitambue,Ishi.
Mwisho.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.