Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesema lishe duni, makuzi na udumavu madhara yake ni makubwa kama watu wote hawatawekeza nguvu kulipatia ufumbuzi.
Ameyasema hayo wakati akisoma hotuba kwenye kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe Kwa kipindi cha Julai - Desemba 2024 na programu jumuishi ya Taifa ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kilichofanyika katika ukumbi wa Chandamali mjini Songea.
"Athari za lishe duni, makuzi, malezi pamoja na udumavu zinaweza zisionekane sasa hivi lakini madhara ni makubwa kama sote hatutoelekeza nguvu kwenye kulipatia ufumbuzi," alisema Kanali Ahmed.
Amesema kuna haja kubwa ya kujiuliza kwa nini Mkoa huu unakuwa na watu wenye udumavu na lishe duni ikiwa unazalisha chakula cha kutosha na cha ziada ambacho kinaenda kuwalisha watu wengine na kupelekea hata kufanya vibaya katika sekta ya Elimu ukilinganisha na mikoa ya jirani Mbeya, Njombe, Lindi na Mtwara.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dr. Louis Chomboko, ametaja faida za lishe bora kwa mtoto ambapo amesema anaweza kufanya vizuri katika masomo, inajenga msingi mzuri wa maendeleo, kuondoa umasikini na uchumi utapanda.
Kwa upande wake Afisa Lishe Mkoa wa Ruvuma, Joyce Kamanga, akiwasilisha tathmini ya lishe amesema hali ya lishe Mkoa wa Ruvuma ni udumavu kwa watoto chini ya miaka 5 asilimia 36.5, uzito pungufu kwa watoto asilimia 12.2, ukondefu kwa watoto asilimia 2.8, upungufu wa damu kwa watoto chini ya miaka 5 asilimia 30 na upungufu wa damu kwa wanawake wenye uwezo wa kuzaa asilimia 45.
Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Manispaa ya Songea na Tunduru DC wametekeleza azimio la mashine kufungwa vinu vya kuongeza virutubishi kwenye unga wa mahindi, na azimio hilo halijatekelezwa katika Halmashauri ya Songea DC, Namtumbo DC, Madaba DC, Mbinga TC na Nyasa DC.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.