MKOA wa Ruvuma umefanikiwa kumaliza chanjo ya kwanza ya UVIKO 19 iliyotolewa na serikali ya Awamu ya sita kwa kuchanja watu 44,000.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma aliyewakilishwa na Dr.Yona Mwakabumbe wakati anatoa nasaha zake kwenye mkesha wa sherehe za Maulid zilizofanyika Msikiti wa wilaya Manispaa ya Songea ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.
Amesema idadi hiyo ya watu waliochanja ni kuanzia Agosti 4 hadi Oktoba 15 mwaka huu ambapo Mkoa umefanikiwa kumaliza chanjo zote na za ziada aina ya JJ ambazo Mkoa ulipewa.
Amewapongeza waumini wa Kiislam kwa kutoa ushirikiano mkubwa wakati wa kutekeleza zoezi la chanjo ya kwanza ambapo amesema watalaam wa afya walikaribishwa kutoa elimu na fursa ya kuchanja kwa waumini.
“Baada ya kumaliza chanjo ya kwanza serikali imetoa chanjo ya pili aina ya sinofam,Mkoa wa Ruvuma tayari tumepata mgawo ni chanjo salama unachoma na kurudia baada ya siku 28’’,alisisitiza Dr Kanga.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Ruvuma,Ustaadh Rajabu Mustapher Songambele,amesema MASJD NUR katika Manispaa ya Songea imetenga hekari 80 kwa ajili ya kujenga shule ambayo itatoa elimu kuanzia chekechea hadi sekondari.
“MASJD NUR imekusudia kuwekeza kwenye elimu ili watoto wetu wapate elimu bora na kuwa katika misingi na maadili mema kwa sababu jamii hivi sasa imepoteza maadili’’,alisisitiza Ustaadh Songambele.
Katika hatua nyingine Katibu huyo wa BAKWATA amesema licha ya elimu,MASJD NUR pia imekusudia ujenzi wa kituo cha afya ndani ya Manispaa ya Songea.
Akizungumza kwenye sherehe hizo,mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amewapongeza waumini wa kiislam kwa maamuzi ya kujenga shule na kituo cha afya ambapo amesisitiza kuwa kwa kufanya hivyo wanaisaidia serikali kuwapatia watanzania elimu na afya.
Amesema serikali ya Mkoa wa Ruvuma, inawaunga mkono katika utekelezaji wa miradi hiyo,hata hivyo ametaka kuwepo na uwazi namna shughuli hizo zitavyofanyika ikiwemo kujua fedha zilizoingia na matumizi yake.
Ametoa rai kwa waumini wa kiislamu na watanzania kwa ujumla kuenzi uzalendo na uhuru wetu kwa sababu Tanzania inayo tunu ya kipekee ya upendo na utangamano ambayo imeifanya nchi kuwa na umoja na amani.
“Hivi vitu viwili umoja na amani tusivichulie kwa urahisi,nayasema haya kwa sababu kabla ya kutaja jina langu naanza na Brigedia Jenerali, ninatambua, nimeshajionea vita maana yake nini, nimeshashiriki, kwenye vita tuilinde amani yetu kama lulu’’,alisisitiza Brigedia Jenerali Ibuge.
Akizungumzia mapambano dhidi ya UVIKO 19 mkoani Ruvuma,Brigedia Jenerali Ibuge amewaongeza waislamu kwa kuzingatia tahadhari za UVIKO 19 ambapo amesema wanafanya vizuri kwenye matumizi ya maji tiririka ambapo amesisitiza pia matumizi ya barakoa.
Hata hivyo amesema miezi miwili iliyopita kabla ya watu kuchanja hali ya corona mkoani Ruvuma ilikuwa mbaya sana, ambapo hivi sasa baada ya watu kuchanja hakuna mgonjwa hata mmoja anayetumia mashine ya kupumulia.
“Idadi ya wagonjwa wanaolazwa kutokana na kupumua imepungua mno,hali hiyo imetokana na mwamko wa kuchanja,hivyo tuendelea kuhamasishana kuchanja chanjo inayokuja ya sinofam’’,alisisitiza.
Mkuu wa Mkoa pia ametoa rai kwa waislam na watanzania wote kwa ujumla kujitokeza katika sensa ya watu na makazi ambayo inatarajia kufanyika Agosti 2022.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Oktoba 19,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.