ZAIDI ya wakazi 1,464 wa Kitai na Ngembambili wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,wanatarajiwa kuondokana na kero ya uhaba wa maji safi na salama baada ya wakala wa usambazaji maji na usafi wa mazingira(RUWASA)kuanza ujenzi wa mradi mkubwa wa maji utakaogharimu zaidi ya Sh.milioni 560.
Mkuu wa Gereza la Kitai Mrakibu wa Magereza Gabriel Rudeligo amesema,kero ya maji safi na salama ni ya muda mrefu kutokana na kukosekana kwa chanzo cha uhakika hivyo kupelekea wakazi wanaoishi katika eneo hilo wakiwemo askari na familia zao kulazimika kutumia maji ya visima vya asili na mito ambayo siyo safi na salama.
Rudeligo,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutoa fedha kwa wizara ya maji na Ruwasa kuanza ujenzi wa mradi huo ambao ukikamilika utamaliza kilio cha muda mrefu cha ukosefu wa maji safi na salama iliyokuwepo tangu Uhuru.
Amesema,kila siku katika eneo la Gereza kuna mkusanyiko mkubwa wa watu hasa wafungwa,wanafunzi wa shule ya msingi,wananchi wanaofika kupata huduma za matibabu kwenye zahanati na familia za askari ambao wanahitaji huduma ya maji ya uhakika kwa ajili ya matumizi ya kila siku .
Mkuu wa Gereza amesema,ni faraja kubwa kama kiongozi wa eneo hilo kuona kilio cha maji sasa kinakwenda kumalizika na kuwapongeza wataalam wa Ruwasa wilaya ya Mbinga na mkoa kwa usimamizi mzuri wa mradi huo.
Ameongeza kuwa,pindi mradi huo utakapo kamilika utawaondolea adha na kero kubwa ya kwenda kutafuta maji kwenye vyanzo vya asili ambavyo havikutosheleza mahitaji yao,hali iliyosababisha baadhi ya shughuli za uzalishaji mali kufanyika kwa kusua sua licha ya nguvu kazi kubwa waliyonayo.
Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa usambazaji maji na usafi wa mazingira(RUWASA)Mhandisi Ruth Koya,amewataka wananchi wanaoishi katika eneo hilo na maeneo ya jirani kuhakikisha wanatunza mradi huo ili uweze kudumu kwa muda mrefu na kuwa suluhisho la changamoto ya maji kwao.
Aidha,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia fedha Ruwasa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji ikiwemo mradi wa maji Kitai ambao unakwenda kutimiza dhamira yake ya kumtua mama ndoo kichwani.
Meneja wa RUWASA wilaya ya Mbinga Mhandisi Mashaka Sinkala alisema,mradi wa maji Kitai utahudumia takribani wakazi 1,468 kati yao 1,204 ni kutoka Gereza la Kitai,shule ya msingi na Zahanati na wakazi 264 kutoka Kitongoji cha Ngembambili ambacho ni maarufu kwa uchimbaji wa madini.Amesema,mradi huo unatekelezwa kwa kutumia wataalam wa ndani na ulianza kutekelezwa mwezi Februari 2023 na ulitakiwa kukamilika mwezi Juni,lakini muda wa utekelezaji wake uliongezwa hadi mwezi Septemba kutokana na sababu za mvua kubwa zilizonyesha na mwingiliano wa kazi hususani za uchimbaji wa mitaro ambazo zilizofanywa na wafungwa wa gereza hilo.
Amelitaja lengo kuu la mradi huo ni kutoa huduma ya maji kwa jamii inayoishi katika eneo na ndani ya gereza la kitai ambalo lilikuwa na uhaba mkubwa wa maji ambapo ukikamilika utasaidia sana kupunguza magonjwa ya mlipuko na kutoa fursa kwa jamii kupata muda wa kushiriki shughuli mbaimbali za kiuchumi.
Amesema,mradi huo utagharimu zaidi ya Sh.milioni 560 na hadi sasa fedha zilizotumika ni Sh.321,710,650.44 sawa na asilimia 57.4 ambazo zimetumika kwa kununua mabomba,tenki na vifaa vingine vya kujengea.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.