SERIKALI ya awamu ya tano imetoa sh.milioni 50 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji kwenye kitongoji cha Mingohi kijiji cha Chimate Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.
Akisoma taarifa ya mradi huo, kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme alipokagua mradi huo,Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) Wilaya ya Nyasa Mhandisi Evaristo Ngole amesema utekeleza wa mradi huo umefikia asilimia 90 ambapo hadi sasa zimetumika zaidi ya sh.milioni 43.
Mhandisi Ngole amesema mradi ulianza kutekelezwa Februari mosi mwaka huu na kwamba kulikuwa na mikataba mitatu ya Utekelezaji wa mradi huo ikiwemo ujenzi wa tanki lenye mita za ujazo 25,000 kwenye chanzo cha maji kwenye milima ya Livingstone.
‘’ Mradi unatekelezwa kwa fedha za wadau wa maendeleo kutoka nchini Uingereza ambao hutoa fedha kupitia Wizara yetu ya Maji chini ya Mpango wa Lipa kutokana na matokeo’’,alisisitiza Ngole.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Isabela Chilumba amesema serikali imetoa zaidi ya sh.milioni 390 za kujenga mradi wa maji katika vitongoji vitatu vilivyobaki vya kijiji cha Chimate ambavyo ni Mtakanini,Chimate kati na Chiwanda.
Amesema tangu kuanzishwa kwa RUWASA Wilaya ya Nyasa imeendelea kutekeleza miradi chini ya program ya maendeleo ya sekta ya maji awamu ya pili ambapo kupitia program hiyo,miradi inatekelezwa kwa fedha za mpango wa lipa kutokana na matokeo.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema ameridhika na Utekelezaji wa mradi wa maji katika kitongoji cha Mingohi ambao amesema umewaondolea kero wananchi ya kutumia muda mrefu kwa kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
‘Mradi wa milioni 50,wanakwenda kufaidika wananchi zaidi ya 1200 kwa kujengewa vituo 12 vya kuchota maji katika kitongoji cha Mingohi ambacho tangu nchi yetu ipate uhuru hawajawahi kupata maji ya bomba,tuna kila sababu ya kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu’’,alisisitiza Mndeme.
Tangu serikali ya awamu ya tano imeingia madarakani kwa Mkoa wa Ruvuma pekee imetoa zaidi ya shilingi bilioni 30 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maji hali ambayo imewaondolea kero wananchi ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
Imeandailiwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Nyasa
Juni 22,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.