WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imetumia zaidi ya shilingi bilioni 2.5 kutekeleza miradi mitatu ya maji.
Meneja wa RUWASA wilayani Mbinga Mhandisi Mashaka Sinkala ameitaja miradi hiyo kuwa ni Pamoja na mradi wa maji Kitai ambao hadi kukamilika unatarajia kutumia shilingi milioni 560.
Amesema mradi huo utahudumia jumla ya wakazi 1,468 kati yao wakazi 1,204 wanatoka katika Gereza la Kitai,shule ya msingi Kitai na zahanati ya Kitai na kwamba wakazi 264 wanatoka katika kitongoji cha Ngembambili.
Mhandisi Sinkala ameutaja mradi mwingine ambao unatekelezwa na RUWASA kuwa ni mradi wa maji kata ya Matiri ambao unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.4
Ameutaja mradi wa maji Matiri kuwa unahusisha vijiji vya Matiri na Kiyaha na kwamba mradi unatarajia kuhudumia wakazi zaidi ya 9870.
Hata hivyo amesema mradi huo hadi sasa umefikia asilimia 60 ya utekelezaji na unatarajia kukamilika Novemba 17 mwaka huu ambapo amesisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutapunguza adha kubwa ya upatikanaji wa maji iliyokuwepo kabla ya kuanza kutekelezwa mradi huo.
“Wananchi wa Matiri kwa muda mrefu wamekuwa wanasumbuliwa na magonjwa ya milipuko kutokana na kutumia maji ambayo sio salama,mradi huu pia utasaidia watu kupata muda mwingi wa kushughulika na kazi zingine za kiuchumi kwa kuwa maji yatakuwa karibu na makazi’’,alisisitiza.
Mradi mwingine ambao unatekelezwa na RUWASA wilayani Mbinga kulingana na Meneja huyo ni mradi wa maji Kitanda unaohusisha vijiji vya Kitanda na Magwangala na kwamba mradi unatarajia kuhudumia jumla ya wakazi 3,600.
Amesema mradi huo unatarajia kutumia zaidi ya shilingi milioni 473 na kwamba mradi umekamilika kwa asilimia 100 na unakwenda kupunguza adha kubwa ya upatikanaji wa maji kwenye vijiji husika.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa RUWASA Tanzania Mhandisi Ruth Koya ameitaja azma ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani inakwenda kutimia miaka michache ijayo.
Amesema anaamini kufikia mwaka 2025 asilimia 85 ya wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini watakuwa wanapata maji safi na salama.
Ameiagiza Menejimenti ya RUWASA kuhakikisha kwamba wakandarasi wanaoidai serikali fedha walipwe mara moja kwa kuwa serikali imeshatoa fedha za kutekeleza miradi hiyo kilichobakia ni taratibu za kuwalipa zikamilike haraka ili wakandarasi wakamilishe kazi zao.
Kaimu Mkurugenzi wa RUWASA Bwai Biseko amesema RUWASA haitaki kujisifia kwa kuhesabu miradi mingapi imetekelezwa badala yake wanapenda kuona namna walivyowagusa wananchi kuhakikisha mradi umekamilika na wananchi wanapata huduma.
Stella Mhagama Mkazi wa Matiri amesema anamshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huo ambapo amesema kwa miaka mingi wanawake na Watoto wamekuwa wanapata kero ya kusafiri kilometa nne kufuata maji mtoni na kubeba kichwani.
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetoa zaidi ya shilingi bilioni 58 katika Mkoa wa Ruvuma kutekeleza miradi 36 ya maji hadi kufikia Juni 30 mwaka huu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.