SERIKALI imetenga shilingi bilioni 22 kuanza kujenga daraja la Mitomoni katika mto Ruvuma linalounganisha wilaya ya Nyasa na Songea mkoani Ruvuma.
Haya yamesemwa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Gofrey Kasekenya wakati anazungumza na wananchi wa Mji wa Mbambabay wilayani Nyasa.
Amesema tayari serikali imelisanifu daraja la mitomoni na Mkandarasi ameshapatikana na kwamba ujenzi wa daraja hilo unatarajia kuanza mwaka huu wa fedha.
Amesema kutokana na umuhimu wa barabara ya Nangombo hadi Chiwindi mwambao mwa ziwa Nyasa mwaka huu serikali imeingiza barabara hiyo kwenye utaratibu wa kufanyiwa upembezi yakinifu na usanifu wa kina.
Hata hivyo amesema barabara ya Mbambabay hadi Lituhi tayari imefanyiwa usanifu wa kina ili hatimaye ianze kujengwa kutokana na umuhimu wa barabara hiyo ambayo ni ya ulinzi na inaunganisha Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Njombe.
Hata hivyo amesema tayari serikali imeifungua wilaya ya Nyasa kwa kujenga barabara ya lami nzito kilometa 66 kutoka Mbinga hadi Mbambabay iliyogharimu zaidi ya shilingi bilioni 129 na serikali ya Awamu ya Sita imekamilisha daraja la mto Ruhuhu lenye urefu wa meta 100 linalounganisha wilaya ya Nyasa Mkoa wa Ruvuma na wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.
Amesema serikali pia inaendelea kujenga barabara ya Lami kipande cha kutoka Kitahi wilayani Mbinga hadi Ndumbi wilayani Nyasa ambako imejengwa bandari ya Ndumbi ambayo imekamilika kwa asilimia 100 na imejengwa shilingi zaidi ya bilioni 12.
“Barabara ya Kitai hadi Ruanda kwa kiwango cha lami inaendelea kujengwa,pia serikali itaendelea kujenga barabara ya lami kutoka Ruanda-Lituhi hadi Ndumbi,Mkandarasi ameshapatikana barabara hiyo inaanza kujengwa kwa kiwango cha lami mwaka huu wa fedha’’,alisema Mhandisi Kasekenya.
Ameongeza kuwa serikali katika mwaka huu wa fedha imetoa shilingi bilioni 70 ili kuanza kujenga upya bandari ya Mbambabay wilayani Nyasa hali ambayo itaiunganisha wilaya ya Nyasa na nchi jirani za Malawi na Msumbiji kupitia ziwa Nyasa.
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mheshimiwa Filberto Sanga ameishukuru serikali kwa kuifungua wilaya ya Nyasa kwa njia ya barabara na majini hali ambayo imemaliza kero ya usafiri na usafirishaji
Amesema Wilaya ya Nyasa imefunguka kupitia ziwa Nyasa,serikali imejenga meli tatu mpya moja ya abiria inayoitwa MV Mbeya II na meli mbili za mizigo zinazoitwa MV Njombe na MV Ruvuma zinazofanya kazi katika ziwa Nyasa kupitia bandari za wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya,Ludewa Mkoa wa Njombe na Nyasa Mkoa wa Ruvuma.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.