WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita haitawatupa wakulima wa tumbaku na amewataka waongeze uzalishaji kwani soko la uhakika lipo.
“Serikali yenu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan haitawatupa mkono, nami kwa maelezo yenu ya leo nitamfikishia salamu Mheshimiwa Rais kuwa mmeazimia mtalima zaidi tumbaku,” amesema.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Oktoba 18, 2022) wakati akizungumza na wadau wa zao la tumbaku wilayani Namtumbo kwenye ukumbi wa shule ya sekondari ya Nasuli, wilayani humo. Wadau hao wanajumuisha wakulima, wanunuzi, wenye viwanda, maafisa kilimo, wasambazaji mbolea na wenye mabenki.
Waziri Mkuu amewapa maagizo viongozi wa mkoa na wilaya wahakikishe kuwa pembejeo za kilimo zinazotolewa na Serikali kwa njia ya ruzuku zinawafikia walengwa na hakuna ubadhirifu unaofanywa.
Akitoa maelekezo kwa viongozi wa mkoa wa Ruvuma, amewataka washirikiane na Wizara ya Kilimo kusimamia upatikanaji wa huduma za ugani kwa wakati ili wakulima waweze kuzalisha kwa tija. “Maafisa Kilimo walio chini ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI na wale walio Wizara ya Kilimo waratibiwe na kusimamiwa kwa pamoja ili wafanye kazi ya kuwahudumia wakulima kwa ufanisi,” amesisitiza.
Akitoa maelekezo kwa Bodi ya Tumbaku, Waziri Mkuu ametaka kuwepo na mikakati madhubuti ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo ili kufikia malengo yaliyowekwa na kusisitiza kuwa wakulima wa tumbaku waelimishwe kufuata mbinu bora za kilimo ili wazalishe kwa tija.
“Bodi ya Tumbaku isimamie upatikanaji wa pembejeo na kuhakikisha zinawafikia wakulima kwa wakati. Kwa kuwa msimu wa uzalishaji wa tumbaku umeanza, pembejeo katika zao hilo ziharakishwe kuwafikia wakulima,” amesisitiza.
Kuhusu malipo kwa wakulima wa zao hilo, Waziri Mkuu ametaka usimamizi wa malipo ya wakulima uimarishwe ili wakulima walipwe kwa wakati. “Masoko ya uuzaji wa tumbaku yaimarishwe sambamba na kutatua changamoto zilizopo ili wakulima wa tumbaku wapate tija zaidi,” ameongeza.
Akitoa maelekezo kwa Ofisi ya Mrajis, Waziri Mkuu amewataka Warajis Wasaidizi wa Mikoa wakutane na viongozi wa vyama vikuu mara kwa mara kupata taarifa ya mwenendo wa vyama vyao. Pia ametaka wakulima wahamasishwe kuwa na umoja na kuimarisha vyama vyao badala ya kuanzisha vyama vingine kwenye maeneo ambayo hayana uhitaji wa kufanya hivyo ilhali vyama vilivyopo vinaweza kuhudumia maeneo hayo.
Akitoa maelekezo kwa Vyama ya Ushirika, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa Chama Kikuu wafuatilie kwa karibu mwenendo wa vyama vya ushirika na kuchukua hatua stahiki kwa wakati. “Vyama Vikuu visimamie kikamilifu vyama vya msingi ili vyama hivyo viweze kutoa huduma stahiki kwa wanachama wao,” amesema.
Mapema, Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Mazao ya Kilimo cha Songea Namtumbo (SONAMCU), Bw. Juma Mwanga alimweleza Waziri Mkuu kwamba chama chao kimeongeza hamasa kwa vyama vya msingi ili wakulima zaidi walime tumbaku na waweze kukidhi mahitaji ya soko.
“Tulikuwa na wanachama 46 lakini katika msimu wa 2022/2023 tumehamasisha vyama vya msingi 62 na vyote vimeahidi kulima zao la tumbaku.”
Pia alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ruzuku ya mbolea ili kumpunguzia mzigo mkulima. “Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa ruzuku ya mbolea kwani bei ya mfuko mmoja ni sh. 70,000 ukienda popote pale hapa wilayani.”
Pia aliomba Serikali ifanye jitihada za makusudi kwa kuajiri maafisa ugani kwenye halmashauri ili wawasaidie wakulima walioko vijijini. Pia aliomba Serikali isaidie kupatikana kwa mikataba (bilateral agreements) baina yake na nchi za Tunisia, Misri na Algeria ambako kuna wanunuzi wakubwa wa tumbaku ya moshi inayozalishwa wilayani humo.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku, Bw. Victor Mwambalaswa alisema kuwa uzalishaji wa tumbaku nchini umeongezeka kutoka kilo milioni 60 hadi kilo milioni 108. “Kimkoa, uzalishaji umeongezeka kutoka kilo 500,000 hadi milioni kilo milioni 9.2.”
Alisema ongezeko hilo la uzalishaji linahitaji kuongezwa kwa miundombinu ya mabani, vichanja na maafisa ugani wa kuwasaidia wakulima.
Naye mbunge wa Namtumbo, Bw. Vita Kawawa alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufungua mahusiano ya kibiashara na nchi za nje hali ambayo alisema imesaidia kupata wanunuzi wa zao hilo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.