Madiwani waagizwa kusimamia miradi
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema serikali itaendelea kutafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wazee zikiwemo kutoa vitambulisho vya matibabu bure kwa wazee.
Kanali Thomas ametoa ahadi hiyo wakati anazungumza na wazee Pamoja na madiwani wa Wilaya ya Mbinga kwa nyakati tofauti katika ukumbi wa sekondari ya Kigonsera na sekondari ya Makita mjini Mbinga.
RC Thomas ametoa rai kwa wazee kuhakikisha changamoto zote zinazowakabili wanazifikisha kwenye Baraza la Wazee la Mkoa wa Ruvuma ambalo limezinduliwa hivi karibuni ili ziweze kutatuliwa kwa haraka.
“Serikali ya Awamu ya Sita ipo tayari kusikiliza na kushughulikia kero mbalimbali za wazee,pia nawaasa vijana hakikisheni mnawahudumia wazee wenu ili mpate baraka kwa sababu wazee ni kudni muhimu ambalo limesahaulika katika jamii ’’,alisisitiza Kanali Thomas.
Ameagiza huduma za afya kuboreshwa katika dirisha la kuhudumia wazee katika kila kituo cha kutolea huduma za afya ili wazee waweze kupata huduma za matibabu kwa haraka.
Mkuu wa Mkoa pia amewaasa wazee kutumika kutatua migogoro inayojitokeza katika jamii na kwamba wazee wanatakiwa kuwa washauri wakuu katika jamii hali ambayo italeta amani na utulivu na vijana kupata fursa ya kujifunza kutoka kwa wazee.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amewaagiza madiwani wa Halmashauri zote kuwa walinzi wa miradi inayotekelezwa katika Kata zao ili iweze kukamilika kwa wakati na ubora unaolingana na thamani ya fedha zilizotumika kwenye miradi husika.
Ameagiza viporo vya miradi ambayo haijakamilika kwa muda mrefu kuhakikisha wanaisimamia na inakamilika ndani ya muda mfupi ili wananchi waanze kunufaika na miradi hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mheshimiwa Aziza Mangasongo akitoa taarifa ya wazee kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,alisema Halmashauri ya Mbinga imewatambua wazee zaidi ya 19,000 hadi kufikia Julai mwaka huu.
Mangasongo amesema wilaya hiyo imeendelea kuwatambua wazee na kutoa vitambulisho vya matibabu kwa wazee ambapo hadi sasa tayari vitambulisho vya CHF iliyoboreshwa vimetolewa katika kaya 4824 zilizojiunga na CHF kati ya kaya zaidi ya 57,000 zilizopo.
Awali wazee wa wilaya ya Mbinga akiwemo mzee Filo Mbepera,Deotela Ndunguru,Anasitazia Hyer ana Emilian Mapunda walizitaja changamoto kuu zinazowakabili wazee na kuiomba serikali kuzipatia ufumbuzi kuwa ni idadi ndogo ya wazee waliopo kwenye mpango wa kaya masikini (TASAF) hivyo kuomba serikali kuongeza idadi ya wazee wanaonufaika na TASAF.
Changamoto nyingine walizitaja kuwa ukosefu wa dawa muhimu za matibabu kwa wazee,baadhi ya wastaafu kuchelewa kupata kiinua mgongo baada ya kustaafu na baadhi ya wazee kuwa hatarini kupoteza maisha kutokana na Imani za kishirikina.
RC Thomas anaendelea na ziara ya kuzungumza na wazee katika wilaya zote tano za Mkoa wa Ruvuma ambapo tayari amezungumza na wazee wa wilaya za Namtumbo na Mbinga.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ruvuma
Septemba 20,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.