Serikali, kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Ruvuma, imetenga mamilioni ya shilingi kwa ajili ya ukarabati wa barabara muhimu zinazounganisha maeneo ya uzalishaji, hususan yale yanayolima kahawa, lengo likiwa ni kurahisisha usafirishaji wa mazao kwenda sokoni. Hatua hiyo inatarajiwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wakulima na jamii nzima ya mkoa wa Ruvuma.
Kaimu Meneja wa TANROADS mkoani Ruvuma, Mhandisi Fedinand Mdoe, alisema barabara ya Nyoni-Mpapa-Mkenda, yenye urefu wa kilometa 108.52, inakarabatiwa kwa Sh milioni 421.26, ambapo kilometa 80.52 zinafanyiwa matengenezo ya kawaida. Aliongeza kuwa kilometa 27 ziko kwenye matengenezo makubwa, ikiwemo kingo za madaraja 3, kwa gharama ya Sh milioni 763.37, na ujenzi wa makalavati 2 unaogharimu Sh milioni 288.05.
Mdoe amezitaja, barabara nyingine zinazofanyiwa matengenezo ni Nyoni-Mpapa-Maguu (kilometa 30) na Mbinga-Mkiri. Alifafanua kuwa, kwenye barabara hiyo, maeneo korofi na miinuko yanawekewa lami ili kuboresha usafiri wa wananchi wa Mbinga na Nyasa. Pia, barabara ya Mbambabay-Lituhi inafanyiwa ukarabati wa dharura, hususan eneo la Lwika, takribani kilometa 15 kutoka Mbambabay, ambapo tuta linainuliwa, box kalavati linajengwa, na changarawe inamwagwa.
Kadhalika, Mdoe alisema barabara ya Nang’ombo-Chiwindi inafanyiwa matengenezo ya dharura kwa kuweka kifusi, lakini changamoto ni magari mazito ya makaa ya mawe, yanayotumia daraja la chuma, jambo linalohatarisha uimara wa daraja hilo. Alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wamiliki wa malori kuzingatia uzito wa mizigo, ili kulinda miundombinu hiyo muhimu. “Tunawasihi makampuni ya makaa ya mawe kuzingatia sheria, kutozidisha uzito wa magari yao, na waangalie maslahi ya umma, si faida yao pekee.” alisema Mdoe.
Kaimu Meneja huyo alihitimisha kwa kusema, kazi nyingi za barabara zinatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka huu wa fedha, na chache zilizosalia, zilizopewa kipaumbele, zitaendelea hadi Septemba 2025. Hatua hizi zinathibitisha azma ya Serikali ya kuboresha miundombinu ya barabara, kuchochea maendeleo ya kiuchumi, na kuboresha maisha ya wananchi wa Ruvuma.
Ukarabati wa barabara hizi ni chachu ya maendeleo, si tu kwa wakulima wa kahawa na makaa ya mawe, lakini kwa jamii nzima ya mkoa wa Ruvuma.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.