SERIKALI imetoa zaidi ya shilingi bilioni sita kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma katika mwaka wa fedha wa 2022/2023.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Neema Maghembe wakati anatoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas alipofanya ziara ya ukaguzi wa miradi katika Halmashauri hiyo.
Maghembe amebainisha kuwa kati ya fedha hizo,Halmashauri imepokea zaidi ya shilingi milioni 735 kwa ajili ya mradi wa uboreshaji miundombinu ya awali na msingi (BOOST),mradi wa vyoo (SWASHI) zimetolewa zaidi ya shilingi milioni 278 na na mradi wa ujenzi wa madarasa ya awali ya mfano (LANES) zimetolewa zaidi ya shilingi milioni 55.
“Halmashauri inapenda kuishukuru serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa namna inavyoendelea kuleta fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri yetu’’,alisema Maghembe.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo,Halmashauri hiyo pia imepokea zaidi ya shilingi milioni 637 kwa ajili ya umaliziaji wa vyumba vya madarasa katika shule za msingi,zaidi ya shilingi milioni 75 kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi ya maendeleo vijijini na kwamba serikali pia imetoa shilingi milioni 440 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi.
Kulingana na Mkurugenzi huyo,serikali imetoa shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya msingi Lizabon na shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vyumba vya madarasa na vyoo.
Fedha nyingine zilizotolewa na serikali katika Halmashauri hiyo ni zaidi ya shilingi milioni 155 ambazo zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya walimu,zaidi ya shilingi milioni 142 kwa ajili ya ujenzi wa bweni sekondari ya Darajambili na chuo cha ufundi Liganga.
Maghembe amezitaja fedha nyingine zilizotolewa ni zaidi ya shilingi milioni 278 kwa ajili ya ujenzi wa vyoo shule za msingi,zaidi ya milioni 362 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa,mabweni na vyoo,milioni 834 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 12,mabweni na vyoo .
Amesema serikali pia imetoa zaidi ya shilingi milioni 751 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ,mabweni na matundu ya vyoo katika sekondari ya Mpitimbi na shilingi bilioni moja zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha wenye ulemavu Kata ya Liganga.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amekagua mradi wa vyoo katika shule ya msingi Parangu uliogharimu shilingi milioni 37,mradi wa ukarabati Kituo cha Walimu (TRC) cha Peramiho kilichogharimu shilingi milioni 22 na mradi wa vyumba vya madarasa ya awali yaliyogharimu shilingi milioni 61 katika Kijiji cha Mpitimbi.
Akizungumza baada ya ukaguzi wa miradi hiyo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amepongeza mradi wa ujenzi wa madarasa ya awali katika Kijiji cha Mpitimbi ambapo ametoa rai kwa wananchi kulinda na kusimamia mradi huo ili uweze kukamilika kwa asilimia 100.
Hata hivyo Kanali Laban hajaridhishwa na utekelezaji wa miradi ya vyoo katika shule ya Parangu na ukarabati wa Kituo cha walimu Peramiho ambapo ameiagiza TAKUKURU kufanya uchunguzi wa kina katika miradi hiyo na kuchukua hatua kwa mtumishi yeyote atakayebainika kuwa na kosa.
Amewataka viongozi kuanzia ngazi ya Kijiji,Kata,Tarafa na Wilaya kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali badala ya kusubiri ziara za viongozi wa Mkoa kufutilia miradi hali inayosababisha miradi kutekelezwa chini ya kiwango.
Amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo Neema Maghembe kuwaandikia barua ya onyo na hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa waandisi wote wanaosimamia miradi kwa sababu wameshindwa kusimamia miradi.
Mwisho
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.