SERIKALI imetoa Sh.milioni 470 kujenga shule mpya ya sekondari katika kijiji cha Amani-Makolo kata ya Amani-Makolo Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma, ili kumaliza kero ya wanafunzi wanaotoka katika kata hiyo kwenda kata ya Mkako umbali wa km 15 kufuata masomo
Awali wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi katika kata hiyo na kuchaguliwa kuendelea na kidato cha kwanza walilazimika kwenda kata nyingine kama vile Mkako,Rwanda na wengine hata shule zilizopo Mbinga mjini kwa ajili ya kuanza masomo ya sekondari.
Kaimu Afisa elimu sekondari wa Halmashauri hiyo Rashid Bundala amesema,kujengwa kwa shule hiyo ni ukombozi mkubwa hata kwa wazazi ambao walilazimika kuwalipia watoto wao gharama ya kusafiri kwenda shule na kurudi nyumbani kila siku.
Amesema,baadhi ya wanafunzi wanaotoka vijiji vya kata hiyo walilazimika kupanga vyumba uraini na kuanza kujitegemea licha ya umri mdogo walionao
Bundala alieleza kuwa,kutokana na changamoto hiyo baadhi ya watoto hasa wa kike walishawishika kuanza mahusiano ya kimapenzi na watu wazima wasiokuwa na maadili mema na hatimaye kushindwa kumaliza masomo kwa kupata mimba na wengine kuchoshwa na umbali uliopo.
Aidha amesema,ujenzi wa shule ya Sekondari Mndeme ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inayotaka kila kata kuwa na shule ya sekondari ili vijana wengi wanaomaliza darasa la saba wapate nafasi ya kuendelea na elimu ya sekondari.
Amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,kutoa fedha ili kujenga shule hiyo sekondari ambayo ni msaada mkubwa kwa watoto wa kata ya Amani-Makolo ambao sasa wanatoka nyumbani na kwenda shule iliyopo karibu na makazi yao.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya Mndeme,wameishukuru serikali kuwajengea shule mpya na kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kwenda katika kata nyingine kufuata masomo.
Solana Adam amesema,wanafunzi wanaotoka katika kijiji hicho walikuwa wakitembea umbali wa kilomita 15 kila siku kwenda na kurudi hadi shule ya sekondari Mkako na kufika wakiwa wamechoka,lakini kwa kujengewa shule hiyo karibu itawafanya kusoma kwa bidii.
Ameiomba serikali kuwajengea mabweni ili wanafunzi hususani wa kike waweze kuishi shuleni ili wapate muda mwingi wa kusoma,badala ya kurudi nyumbani ambako wanakutana na kazi nyingi zinazowakosesha kupata muda wa kujisomea.
Hadija Mustapha amesema changamoto kubwa ni maji safi na salama,kwani licha ya kuwepo kwa mtandao wa maji lakini yanayotoka hayafai kwa matumizi ya binadamu kwa kuwa yanatope jingi hivyo wanalazimika kutumia maji ya mvua yanatoka juu ya bati za nyumba.
Ameiomba wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilaya ya Mbinga,kuboresha huduma zake ili kuwaepusha wanafunzi na walimu wa shule hiyo uwezekano wa kupata magonjwa mbalimbali ikiwamo ya matumbo na kipindupindu.
Mkuu wa shule hiyo Deniterias Mgaya amesema,katika mwaka wa masomo ulioanza tarehe 9 Januari, walipangiwa kupokea wanafunzi 184 wa kidato cha kwanza kati yao wavulana 75 na wasichana 105,na hadi kufikia wiki iliyopita wanafunzi 26 bado hawajaripoti.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.