SERIKALI ya awamu ya tano inatekeleza mradi wa ujenzi wa daraja la Ruhuhu lenye urefu meta 98.01 linalounganisha Mkoa wa Ruvuma na Njombe kwa gharama ya shilingi bilioni 6.172.
Mradi huo ambao ujenzi wake umechukua muda mrefu kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya mafuriko ya mto Ruhuhu unamwaga maji yake ziwa Nyasa.
Meneja wa Wakala wa Barabara TANROADS mkoani Ruvuma Mhandisi Lazeck Alinanuswe anasema ujenzi umefikia zaidi ya asilimia 85 ambapo nguzo tatu kati ya nne zilizojengwa ndani ya mto Ruhuhu zimekamilika.
“Ni kweli mradi umechukua muda mrefu, wakati wa mvua za masika mradi ulisimama kutokana na mafuriko ya mto Ruhuhu na baada ya Mvua kupungua mkandarasi ameendelea kukamilisha kazi ya kujenga nguzo moja sehemu iliyobakia’’,anasema Mhandisi Alinanuswe.
Mkataba wa ujenzi wa nguzo nne za daraja ulisainiwa mwaka 2016 kati ya Mkandarasi wa Kampuni ya M/s Lukolo na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa gharama ya sh bilioni 6.17 na muda wa utekelezaji ni miezi 24.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma anasema mradi huo umekuwa unamnyima usingizi kwa kuchelewa kukamilika na kwamba mradi umechukua mrefu kukamilika hasa katika kipindi cha mvua za masika ambapo mto Ruhuhu unafurika na kusababisha Mkandarasi kushindwa kuendelea na kazi.
“Kazi inayoendelea na Mkandarasi ya kumalizia nguzo moja ambayo inatakiwa kujengwa katikati ya mto Ruhuhu,haiwezi kuendelea wakati mto umefurika,hivyo ujenzi umeanza baada ya mvua kupungua’’,anasema Mndeme.
Anabainisha zaidi kuwa Mkandarasi akishamaliza kazi ya kujenga nguzo moja iliyobakia,ndipo kazi ya kutandaza vyuma na nondo juu ya daraja kupitia nguzo nne itafanywa na TANROADS wenyewe.
“Namuomba Mkandarasi wa daraja hili kufanya kazi hiyo kwa kasi ,ufanisi na ubora ili wananchi wa wilaya za Nyasa mkoani Ruvuma na Ludewa mkoani Njombe waanze kunufaika kupitia daraja hili’’,anasisitiza Mndeme.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Agosti 24,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.