Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amewaagiza wakuu wa shule za msingi na sekondari kuhakikisha wanainua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi na kuunasua Mkoa kwenye ufauli usioridhisha ambao umedumu kwa kipindi cha miaka mitatu.
Kanali Thomas ametoa agizo hilo wakati anazungumza kwenye kikao kazi na walimu wakuu wa shule za msingi na wakuu wa shule za sekondari kilichofanyika kwa nyakati tofauti kwenye ukumbi wa sekondari ya Songea.
“Mtambue kuwa sisi viongozi wenu hatupo tayari kuuona Mkoa unaendelea kufanya vibaya katika sekta ya elimu,hivyo tumieni kikao hiki kuwa chachu ya kufanya mabadiliko,mwaka huu tuanze kwa kufanya mabadiliko makubwa katika utendaji wetu wa kazi ’’,alisisitiza RC Thomas.
Ametahadharisha baada ya kikao hicho hatasikiliza kisingizio chochote kwa matokeo yasiyoridhisha kwenye mitihani ya kitaifa ambapo amewaagiza wakuu hao kujirekebisha na kufanya tathmini ya utendaji kazi ili kuongeza uwajibikaji.
Ili kuhakikisha ufaulu katika elimu ya msingi na sekondari unaongezeka Mkuu wa Mkoa amewaagiza wakuu wa shule kusimamia na kuinua taaluma katika shule zao.
Mkuu wa Mkoa pia ameagiza miradi ya ujenzi kusimamiwa ipasavyo na kusimamia fedha za serikali zinazotolewa kwa uendeshaji wa shule.
Maagizo mengine ambayo ameyatoa ni kila shule kupanda miti ya matunda,kushirikiana na jamii katika kuleta maendeleo ya shule,kuboresha mazingira ya shule,kujiepusha na mikopo inayotolewa na Taasisi zisizo za kibenki na kutekeleza agizo la kila shule kulima hekari tano za mazao ya nafaka,mbogamboga na matunda.
Awali akitoa taarifa ya elimu ya msingi na sekondari kwenye kikao hicho,Afisa Elimu wa Mkoa wa Ruvuma Mwl,Edith Mpinzile amesema Mkoa umeendelea kufanya vibaya kwenye matokeo ya mtihani wa kitaifa kwa kuwa Mkoa umeshindwa kufikia lengo la ufaulu lililowekwa kitaifa la asilimia 85 kwa mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi na asilimia 100 ya upimaji wa mitihani ya darasa la nne.
Ameutaja ufaulu wa darasa la saba mwaka 2023 ulikuwa ni asilimia 69.9 na ufaulu wa darasa la nne ni asilimia 76.01 ambapo amesema Mkoa pia umeendelea kufanya vibaya katika mitihani ya sekondari ya kitaifa kwa kuwa Mkoa umeshindwa kufikia lengo la ufaulu la asilimia 100 kwa mtihani wa upimaji wa kidato cha pili ambapo ufaulu wa Mkoa mwaka 2023 ulikuwa ni asilimia 81.96.
Hata hivyo amesema Idara ya Elimu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imebaini mambo mbalimbali yanayosababisha ufaulu usioridhisha ambayo ameyataja kuwa ni baadhi ya walimu wanashindwa kutekeleza majukumu yao ya kila siku,mada hazikamilishwi na walimu hawatoi mazoezi na majaribio ya kutosha.
Changamoto nyingine amezitaja kuwa ni baadhi ya walimu hawazungumzi na wanafunzi kujua changamoto zao,walimu hawakai kwenye vituo vya kazi,walimu hawana ubunifu na walimu kuwa na madeni yaliyopitiliza ambayo yanaondoa utulivu kazini hivyo walimu wanashindwa kufundisha kikamilifu.
Mkoa wa Ruvuma una shule za msingi 841 na shule za sekondari 233
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.