Katika kipindi cha miaka minne, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imepiga hatua kubwa za maendeleo, ikiwa ni matokeo ya uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Mheshimiwa Michael Mbano, ameishukuru Serikali kwa kupeleka zaidi ya shilingi bilioni 188 kuboresha huduma na miundombinu ya maendeleo.
Sekta ya Elimu Yapata Upekee
Elimu imekuwa miongoni mwa sekta zilizopata msukumo mkubwa, ambapo jumla ya madarasa 244 yamejengwa kwa thamani ya shilingi bilioni 5.23.
Sanjari na hilo, shule nne mpya za sekondari zimejengwa, ikiwemo shule ya Dkt Lawrance Gama, Luhira Sekondari, Dkt Damas Ndumbaro na shule maalumu ya Amali katika kata ya Ruvuma, kwa gharama ya bilioni 3.6.
Katika kuhakikisha elimu inapatikana kwa wote, Halmashauri pia ilitumia shilingi milioni 800 za mapato ya ndani kujenga shule maalumu ya awali na msingi kwa mchepuo wa Kiingereza, ambayo ilizinduliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 24 Septemba 2024. Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 491.
Zaidi ya hayo, mpango wa elimu bure unaendelea kuimarika, ambapo kila mwezi Manispaa hupokea shilingi milioni 298 kwa ajili ya kuendesha shule za msingi na sekondari.
Katika kipindi cha miaka minne, sekta ya elimu imepokea jumla ya shilingi bilioni 14.24.
Huduma za Afya Zaimarika
Sekta ya afya imepokea shilingi bilioni 6.73, ambapo shilingi bilioni 5 zimetumika kujenga Hospitali ya Manispaa ya Songea, vituo vya afya vinne na zahanati nne.
Aidha, shilingi bilioni 1.735 zimetengwa kwa ajili ya matibabu, huku bajeti ya kila mwezi ya dawa na vifaa tiba ikipanda kutoka milioni 18 hadi milioni 40.7.
Maji ya Uhakika kwa Wakazi wa Songea
Huduma ya maji imeboreshwa kutoka asilimia 82 hadi 92, huku mradi wa maji wa bilioni 145.7 kwa miji 28 ukiwa mwokozi wa upatikanaji wa maji Manispaa ya Songea.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutuletea mradi huu, ambao ukikamilika utafikisha upatikanaji wa maji asilimia 100,” alisema Meya Mbano.
Miundombinu Yaimarishwa
Katika sekta ya barabara, Manispaa ya Songea imepokea shilingi bilioni 22 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami nzito zenye urefu wa kilomita 10.1 katika kata za mjini.
Mradi huo tayari umefikia asilimia 89 ya utekelezaji. Aidha, ujenzi wa stendi kuu ya mabasi ya Songea umekamilika kwa gharama ya shilingi bilioni 6.5.
TASAF na Ruzuku ya Mbolea zilivyoboreshs Maisha ya Wananchi
Kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF), bilioni 9 zimetolewa kwa kaya maskini, huku asilimia 60 ya wakazi wa Songea wakifaidi ruzuku ya mbolea.
Tani 88,208 za mbolea zimetolewa kwa wakulima, hatua iliyosaidia kuongeza uzalishaji wa chakula na kuboresha uchumi wa kaya.
Mikopo kwa Makundi Maalum na Ukuaji wa Mapato
Katika kipindi cha miaka minne, shilingi bilioni 2.2 zilitolewa kama mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Manispaa pia imepata kibali cha kutoa mikopo kupitia Benki ya NMB, ambapo shilingi bilioni 1.3 zipo katika hatua za kukopeshwa.
Kwa upande wa mapato ya ndani, ukusanyaji umeongezeka kutoka shilingi bilioni 2.1 hadi bilioni 6.8, huku bajeti ya mwaka 2025/2026 ikitarajiwa kufikia bilioni 9.
mafanikio haya ni ushahidi wa jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha maisha ya wananchi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.