TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma imeokoa zaidi ya shilingi 359 katika kipindi cha kuanzia mwezi Aprili hadi Juni mwaka huu.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Owen Jasson amewaambia wanahabari wakati anatoa taarifa ya Taasisi hiyo ya miezi mitatu kuwa kati ya fedha zilizookolewa zaidi ya shilingi milioni 283 ni marejesho ya fedha za vyama vya ushirika na SACCOS katika wilaya za Songea,Mbinga na Namtumbo.
Kulingana na Jasson zaidi ya milioni 13 zimeokolewa kutokana na ufuatiliaji wa makusanyo ya fedha za vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo katika wilaya za Tunduru na Mbinga na shilingi milioni 36 ni marejesho ya fedha za Benki ya wananchi wa Mbinga.
“Katika kipindi tajwa TAKUKURU Ruvuma imefanya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo nane ili kujiridhisha iwapo fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo zimetumika kadri ilivyokusudiwa na kunakuwa na thamani ya fedha’’,alisisitiza Jasson.
Ameitaja miradi iliyofuatiliwa kuwa ipo katika sekta za miundombinu na afya ikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.8 nakwamba miradi hiyo ni ujenzi wa vituo vya afya Magagura,Mtakanini na Matimira kila kimoja kikiwa na thamani ya shilingi milioni 400.
Miradi mingine ni matengenezo ya barabara ya Maposeni hadi Likingo yenye thamani ya shilingi zaidi ya milioni 230,matengenezo ya barabara ya Mageni hadi Rwinga wilayani Namtumbo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 158 na barabara ya Libango hadi Kiburungutu wilayani Namtumbo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 181.
Amesema katika uchunguzi wa miradi hiyo ilibainika alama za barabarani katika matengenezo ya barabara ya Maposeni hadi Likingo wilayani Songea zilikuwa hazijawekwa na kwamba kuna kipande cha kilometa tatu ambacho kilitakiwa kuwekwa kifusi lakini hakikuwekwa,hivyo TAKUKURU ilimwelekeza Mkandarasi kukamilisha kazi hiyo na ufuatiliaji unaendelea.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Juni 18,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.