Tamasha la Maonesho ya Vita ya Majimaji na Utalii wa Uhifadhi wa Utamaduni limezinduliwa rasmi mkoani Ruvuma, likiwa na lengo la kuenzi historia ya vita hivyo na kukuza utalii wa utamaduni.
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Mhe. Pares Magiri, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesisitiza kuwa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa yenye rasilimali nyingi, ikiwemo ardhi yenye rutuba, madini, na hifadhi za wanyama.
Shughuli mbalimbali zimepangwa kufanyika katika tamasha hili, likianza na maonesho ya taasisi za serikali na sekta binafsi tarehe 23 Februari 2025, katika viwanja vya Makumbusho ya Majimaji.
Tarehe 25 Februari, mdahalo wa wadau utafanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Namtumbo, kisha kutembelea kijiji cha Maposeni, makazi ya Chifu Emmanuel Zulu II wa Wangoni, pamoja na Machifu kutoka mikoa mbalimbali.
Sherehe za Ngoni Day zitafanyika tarehe 26, zikijumuisha vyakula vya asili, ngoma, nyimbo, na maonesho ya filamu kuhusu mchango wa wanawake katika uhifadhi wa urithi wa utamaduni.
Maadhimisho hayo yatafikia kilele chake tarehe 27 Februari 2025, katika eneo la gereza la kwanza la Wajerumani lililojengwa kati ya 1897 na 1902, ambapo kumbukizi ya Nduna Mkomanile, mwanamke aliyepigana na kunyongwa wakati wa vita vya Majimaji, itafanyika.
Mgeni rasmi katika kilele cha Kumbukizi hizo anatarajiwa kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania, Jenerali Jacob John Mkunda. Wananchi wote wamehimizwa kushiriki kwa wingi katika maadhimisho haya ya kihistoria.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.