Tanzania inahitaji uwekezaji zaidi wa mashamba makubwa ya kilimo ili kufungua fursa za ajira kwa wananchi, kukuza uchumi na kuongeza mapato ya fedha za kigeni kupitia mauzo ya mazao nje ya nchi. Mfano bora wa mafanikio hayo ni Shamba la Kahawa la Aviv Tanzania Limited lililopo Kijiji cha Lipokela, Wilaya ya Songea, Mkoa wa Ruvuma, ambalo limeajiri maelfu ya Watanzania na kuongeza mchango wa zao la kahawa katika uchumi wa Taifa.
Shamba la Aviv lina ukubwa wa zaidi ya hekta 2,000 na huzalisha kahawa bora inayoitangaza Tanzania kimataifa. Meneja wa shamba hilo Hamza Kassim amesema Aviv inachangia asilimia 4.5 ya kahawa yote inayozalishwa nchini, huku asilimia 60 ya kahawa hiyo ikiuzwa moja kwa moja nje ya nchi. Aidha, shamba hilo limeanza kuzalisha pilipili manga kwa mauzo ya nje, hatua inayoongeza mapato ya fedha za kigeni.
Kwa mujibu wa Meneja Msaidizi wa Kampuni hiyo, Muthana Maruvanda, Aviv imewekeza katika miundombinu bora ya umwagiliaji ambayo imekuwa chachu kwa wakulima wa Ruvuma kujifunza kilimo cha kisasa, jambo linalowezesha kuimarika kwa uzalishaji na ubora wa kahawa mkoani humo. Aviv pia hutoa ajira za kudumu zaidi ya 1,400 na ajira za msimu zaidi ya 5,000 kila mwaka.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipotembelea shamba hilo Septemba 2024, alisema mafanikio makubwa katika sekta ya kilimo si bahati mbaya bali ni matokeo ya sera bora na juhudi kubwa za Serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na kurudisha masoko ya mazao. Rais Samia alisisitiza umuhimu wa mashamba makubwa kushiriki katika shughuli za kijamii, ikiwemo uchimbaji wa visima kwa ajili ya umwagiliaji.
Takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa uzalishaji wa kahawa umeongezeka kutoka tani 60 hadi tani 85, huku mauzo ya zao hilo nje ya nchi yakiingiza dola milioni 250. Serikali inaamini kuwa uwekezaji zaidi wa mashamba kama Aviv utazidi kuinua sekta ya kilimo, kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kuondoa changamoto ya ajira kwa vijana nchini.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.