Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imesema inatarajia mafunzo yanayotolewa kwa watendaji ngazi ya mkoa kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yatawasaidia kupata elimu na ujuzi wa kutosha utakaowawezesha kutekeleza majukumu yao ili kufanikisha uboreshaji wa Daftari.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Daftari na TEHAMA, Bw. Stanslaus Mwita, wakati akisoma hotuba kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe. Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele, akifungua mafunzo kwa watendaji ngazi ya mkoa kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Ruvuma, uliofanyika katika ukumbi wa Chandamali mjini Songea.
"Baadhi yenu mlibahatika kushiriki katika kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Tume ikiwemo uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika awamu zilizopita, kwa kutumia uzoefu mlionao na mafunzo mtakayopatiwa ninaamini mtafanya kazi zenu kwa weledi, bidii na moyo wa kujituma ili kufanikisha zoezi hili," alisema Mwita.
Hata hivyo amewakumbusha kuwa matokeo bora ya zoezi hilo yanategemea uwepo wa ushirikiano kati ya watendaji wote wa uboreshaji wa Daftari ikiwemo Serikali, vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi, pia kuwa na ushirikiano mzuri na wa karibu na Tume wakati wote wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Naye Kaimu Mkurugenzi na Afisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Andrew Mbunda, amesema wameshajipanga vizuri kwa kuwa wameshafanya usahili wa waendesha vifaa na waandishi wa uboreshaji wa Daftari na kupokea vifaa mbalimbali kutoka Tume Huru ya Uchaguzi, hivyo baada ya mafunzo, nao wataenda kutoka mafunzo hayo kwa wasaidizi ngazi ya Kata.
Kwa upande wake Afisa Uchaguzi wa Jimbo la Songea mjini, Buruhani Mapunda, ametoa wito kwa wananchi wa Manispaa ya Songea na maeneo mengine kwa wale ambao hawajawahi kujiandikisha na wana vigezo, kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, na wanaotaka kuboresha au waliohama kutoka eneo moja kwenda jingine wajitokeze kuhamisha taarifa zao ili wasomeke katika vituo vyao vya sasa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.