TUME ya Taifa ya Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi (National Land Use Planning Commisio-NLUPC) imeendesha zoezi la kupendekeza, kutathmini na upimaji wa ardhi kwa matumizi mbalimbali katika Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Mpango huu wa Tume umepitia katika vijiji nane katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ambavyo ni kijiji cha Muhuwesi, Liwangula, Ngapa,Chawisi, Mnazi mmoja,Matemanga,Ligunga na Jaribuni.
Lengo la zoezi hilo ni kuboresha matumizi ya ardhi nchini kwa kuweka mpango madhubuti unaolinda na kusimamia rasilimali ardhi kwa ajili ya matumizi endelevu. Zoezi hili litasaidia kukabiliana na migogoro ya ardhi baina ya watumiaji mbalimbali, vile vile kuwezesha upatikanaji wa Ardhi kwaajili ya uwekezaji katika maeneo hayo.
Akizungumza Bi Pili Msati ,Msimamizi wa kanda nyanda za juu Kusini -(NLUPC), alieleza kuwa , lengo la Serikali ni kujenga uelewa kwa wananchi wa maeneo ambayo yana muingiliano wa matumizi ya ardhi ,ili kuweka matumizi bora na sahihi ya ardhi kwa watumiaji tofauti.
"Tume imekuja kuwezesha mipango kwa lengo la kuweka sawa wastani wa matumizi ya ardhi,lazima tuhakikishe kwamba wananchi wanaishi kwa kuheshimu hifadhi na sehemu zote za ardhi zilizotengwa kwa matumizi maalumu”. Alisema.
Aidha Mpima Ardhi (W) Tunduru Ndg. Jeremia Nhambu, ameishukuru Serikali kwa kuleta mpango huu, kwani litasaidia kukabiliana na migogoro ya matumizi ya ardhi baina ya watumiaji mbalimbali hasa ya wafugaji na wakulima kwa njia ya Amani na haki. Pia, ameongezea kwa kuwakaribisha wawekezaji kwani mpango huu unaainisha maeneo ya uwekezaji katika maeneo yaliyoainishwa.
Pia kwa upande wao wananchi wa vijiji vilivyopitiwa na mpango huo ,wameishukuru Serikali kwa mpango huo kwani utapunguza migongano kati ya wakulima na wafugaji, pia wamehaidi kulinda na kufuata mpango huo wa Matumizi Bora ya Ardhi.
Mpango mzuri wa matumizi ya ardhi unaweza kuvutia wawekezaji kwa kutoa mwongozo wa maendeleo ya muda mrefu. Hii inawahakikishia wawekezaji kuwa siasa ya ardhi za eneo hilo ni thabiti na ina misingi ya kisheria, ambayo inaongeza Imani yao katika uwekezaji.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.