HALMASHAURI ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,imeanza kujenga ofisi za kisasa kwa kila kijiji zitakazotumika kutoa huduma bora kwa wananchi na kupanua wigo wa kuongeza mapato ya Halmashauri na Serikali kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Hairu Musa,alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa ofisi ya kijiji cha Tuleane kata ya Mchangani ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 95.
Alisema,wilaya Tunduru ina vijiji 157 ambavyo vinakwenda kupata ofisi za kisasa kwa ajili ya maafisa watendaji ambao watashirikiana na watumishi wengine wa Halmashauri kukusanya mapato ya ndani kwa asilimia 100.
Alisema,katika mkakati wao wa kukusanya na kuongeza mapato ya ndani,wameanza kuboresha maeneo ya kazi ambayo yatakuwa rafiki,kuchochea ari ya kazi na uwajibikaji kwa watumishi.
Kwa mujibu wa Hairu ni kwamba,hatua hiyo itasaidia sana Halmashauri kuwa na uwezo wa kujiendesha na kutoa huduma bora za kijamii, badala ya kutegemea mapato kutoka Serikali kuu.
Hairu ambaye ni Diwani wa kata ya Mchangani alisema,kata yake ina vijiji vitano,kati ya hivyo vijiji vitatu wananchi kwa kushirikiana na Halmashauri wamekamilisha ujenzi wa ofisi na matarajio yao ifikapo mwaka 2025 vijiji vilivyobaki vipate ofisi mpya.
Hairu amewataka viongozi kuanzia ngazi za vijiji na kata,kuwashirikisha wananchi katika maeneo yao kuibua miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa zahanati,vituo vya afya,miradi ya maji ,miundombinu ya barabara na ofisi za vijiji ili kuharakisha maendeleo na kukuza uchumi.
Amewaomba wadau wakiwemo wafanyabiashara,madiwani na wabunge wa Jimbo la Tunduru Kusini na Kaskazini,kuunga mkono kwa kuchangia ujenzi wa ofisi za vijiji ambazo ni chanzo mojawapo cha mapato.
Kwa upande wake mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Tuleane Said Goloka alisema,awali walilazimika kutumia nyumba ya mwananchi kuendesha shughuli zao,hata hivyo changamoto kubwa ilikuwa kipindi cha masika kwani nyumba hiyo ilikuwa mbovu.
Alisema,hali hiyo iliwalazimu watumishi wa serikali ngazi ya kijiji kutoka nje kila inaponyesha mvua ili kukwepa kuangukiwa na paa la nyumba kutokana na uchakavu wake.
Goloka,ameipongeza serikali kupitia Halmashauri ya wilaya kuanzisha ujenzi wa ofisi mpya za kijiji na kueleza kuwa ,zitasaidia kuchochea maendeleo na kuhamasisha wananchi kupenda kushiriki na kujitolea nguvu zao katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.