UJENZI wa Barabara ya Mbinga –Mbambabay mkoani Ruvuma yenye urefu wa kilomita 66 iliyojengwa kwa kiwango cha lami na Kampuni ya Chico kwa gharama ya Sh.bilioni 129,361,352,517.84 imekamilika na kuanza kutumika.
Mhandisi Mwandamizi wa miradi kutoka ofisi ya wakala wa Barabara nchini(Tanroads)mkoa wa Ruvuma Justine Mrope alisema, ujenzi wa barabara hiyo ulianza mwezi April 2018 na kukamilika rasmi mwezi Januari 2021.
Mrope alisema,kukamilika kwa Barabara hiyo kutaleta maendeleo makubwa katika wilaya ya Mbinga,Nyasa na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla kwa kuwa wakulima wengi wataweza kusafirisha mazao na bidhaa mbalimbali.
Alisema, mradi huo wa barabara ya Mbinga-Mbambabay unajumuisha na ujenzi wa mizani katika eneo la Buluma ambayo imekamilika kwa ajili ya kusaidia kudhibiti uzito wa magari,hata hivyo haijaanza kutumika kutokana na kukosa watumishi.
Kwa mujibu wa Mrope, kabla ya barabara ya Mbinga-Mbambabay kujengwa kulikuwa na changamoto nyingi ikiwamo baadhi ya akima mama wajawazito kujifungulia njia kabla ya kufika zahanati na vituo vya afya kutokana na umbali na ubovu wa barabara,lakini sasa changamoto zimemalizika.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Tanroads mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha ambazo zimewezesha kumaliza ujenzi wa barabara hiyo ambayo inakwenda kuchochea kukua kwa uchumi wa wananchi wa wilaya hizo.
“kwa kweli napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru sana Rais Samia Hassan kwa kuendelea kutupatia fedha ili kuendelea na kazi za matengenezo ya barabara,ujenzi na ukarabati wa barabara ,makalavati na madaraja katika mkoa wetu” alisema.
Aidha alisema, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Tanroads mkoa wa Ruvuma imeidhinishiwa jumla ya Sh.bilioni 23.742 kwa ajili ya matengenezo ya barabara na madaraja.
Mlavi alisema,Tanroads mkoa wa Ruvuma inalo jukumu la kusimamia matengenezo ya mtandao wa Barabara wenye urefu wa kilometa 2,166.62 kati ya hizo Barabara kuu zina urefu wa kilometa 920.98 na Barabara za mkoa zina urefu wa kilometa 1,245.65.
Alisema, kati ya kilometa 920.98 za Barabara kuu,kilometa 702.60 ni za lami na kilometa 218.38 ni changarawe na wanaendelea kufanya kazi za matengenezo ya barabara,ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja, na usimamizi wa hifadhi za barabara na mizani.
Alisema, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Disemba 2021 jumla ya mikataba 47 imesainiwa na matengenezo ya barabara kuu na barabara za mikoa yalikamilika kwa asilimia 57 za utekelezaji wake.
Mkazi wa wilaya ya Mbinga John Millanzi,ameipongeza wizara ya ujenzi kwa kumaliza changamoto ya barabara na Tanroads kwa usimamizi mzuri ambao umefanikisha kujengwa kwa viwango na kukamilika kwa muda uliopangwa.
MWISHO
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.