MOJA ya vivutio vya utalii wa kiutamaduni vinavyopatikana katika kijiji cha Mbingamharule wilaya ya Songea mkoani Ruvuma ni uwepo wa kaburi la duara ambalo Chifu Nkosi Mharule bin Zulu Gama alizikwa mwaka 1889.
Mambo ambayo yanawashangaza wengi wanaotembelea kaburi hili ni historia inayoonesha kuwa Nkosi Mharule baada ya kufariki alizikwa kwa desturi na mila za kichifu za kabila la wangoni toka Afrika ya kusini.
Christian Ngonyani mwenye umri wa miaka 87 ni mzee wa Mila katika kijiji cha Mbingamharule anasema kijiji hicho kimepewa jina la chifu huyo ambaye alitokea nchini Afrika ya kusini na kutawala ungoni kuanzia mwaka 1847 hadi 1889 alipofariki na kuzikwa katika kijiji hicho.
“Chifu Mharule baada ya kufa mwaka 1889 alizikwa kwa taratibu za jadi ya machifu wa Afrika ya kusini,kaburi lake lilikuwa la mviringo,sanda yake ilikuwa ya ngozi ,alikarishwa kwenye kiti cha ngozi,walikamatwa watu wawili wakiwa hai walizikwa naye wakiwa wamesimama mbele na nyuma ya chifu’’,alisimulia mzee Ngonyani.
Amezitaja taratibu za kijadi za wakati huo zilitaka Mfalme au Chifu anapofariki ni lazima azikwe na watu wawili wakiwa hai na kusisitiza kuwa hiyo ilikuwa ni amri ya serikali ya jadi na hapakuwepo mtu aliyepinga.
Mzee Ngonyani amewataja wengi waliokuwa wanazikwa wakiwa hai na Mfalme ni wale ambao walikuwa wamezoeana na kufanyakazi naye kwa karibu.
Hata hivyo amesema kaburi hilo linatumiwa na wananchi wa kijiji hicho kwenda kuhiji kila mwaka kwenye kaburi hilo ambalo lipo kilometa mbili toka kijijini hapo na kwamba ndugu wa Chifu Mharule toka Afrika ya Kusini huwa wanafika kufanya matambiko kwenye kaburi hilo.
Amesema mwaka juzi ukoo wa Mharule toka Afrika ya kusini walifika kushuhudia kusimikwa kwa Chifu Nkosi Imanuel Zulu Gama wa Tano ambaye ndiyo chifu wa wangoni wa sasa.
Amesema yeyote ambaye anapenda kwenda kutembelea kaburi hilo kuna taratibu zake za kimila ambazo amezitaja kuwa ni kubeba unga wa muhogo,mahindi na ulezi ambao unatengenezwa na bibi katika kijiji hicho.
Baada ya kufika eneo la kaburi anatangulia mhusika ambaye anawasiliana na chifu kwa lugha ya jadi ndipo wanaoitwa waliofika kutambika na kupiga magoti juu ya kaburi na kuomboleza kwa sala za jadi.
“Baada ya maombi kuku au mbuzi wanachinjwa juu ya kaburi la Chifu Mharule,jambo la kushangaza mbuzi anapochinjwa hapigi kelele,baada ya kuchinja mmoja anamwaga unga wote juu ya kaburi’’,anasema.
Hata hivyo anasema ukifika asubuhi juu ya kaburi hauoni damu wala unga vyote vinakuwa vimeliwa na kwamba hiyo ndiyo ishara ya kukubaliwa shida zote ambazo ulikwenda kuomba kwenye kaburi hilo.
Agnes Ngonyani Msaidizi wa Mzee Ngonyani amesema wanapokea wageni wengi wanaotembelea kaburi la Chifu Mharule kutoka nchi za Ulaya,Marekani na Afrika ambao wanakwenda kwa shida mbalimbali ikiwemo kuhiji na kufanya matambiko.
“Nimekuwa nawapeleka watu wa kawaida,waganga wa jadi,watalii na wagonjwa wanaenda kufanya maombi kwenye kaburi la Chifu na kufanikiwa’’,anasema Ngonyani.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Machi 8,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.