UTALII WILAYA YA NYASA UNAANZIA KATIKA JINA LA MBAMBABAYMbambabay mji ambao ni makao makuu ya wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma,kulingana na Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe jina la “Mbamba bay,” ni kwamba Mbamba lina maana ya radi na bay ikimaanisha ghuba.
Mbambabay ni Kitovu cha utalii mkoani Ruvuma kwa kuwa ni mji wenye vivutio vya utalii vya kila aina,vivutio vyenye historia ya kupendeza na kuvutia kwa wageni.
“Tafsiri hizi ambazo zilitolewa na wenyeji zinasema wakati wa zamani kutokana na radi kali za mara kwa mara kupiga kwenye Rasi iliyopo karibu na Ghuba hiyo na ndipo eneo likaitwa Mbamba bay’’,anasisitiza Challe.
Challe anabainisha Zaidi kuwa Rasi hiyo ni kubwa na imefunikwa na uoto wa asili wa miti na nyasi, baadhi ya miti hiyo inatumika kama dawa za asili hadi sasa.
Wakazi wa eneo hilo hutumia msitu wa Mbamba kwa matambiko ya kupiga ngoma za kufukuza au kuita majini kwa imani zao na kwamba katika msitu huo kuna wanyama kama chui ambao hutokea milima ya Nangombo, Ukuli na Chinyemba ambao wanapatikana katika rasi hiyo,wakiwafuata wanyama aina ya ngedere waliopo kwa wingi katika msitu huo.
Mbunge wa Jimbo la Nyasa Mhandisi Stella Manyanya anataja moja ya ngoma maarufu wilayani humo ni Mganda,ngoma hii inachezwa na wanaume na ngoma ya Kioda ambayo inachezwa na akina mama.
Ngoma nyingine maarufu wilayani Nyasa ni kama vile Lindeku, Mhambo, Lingoga na Chomanga ambazo wanacheza mchanganyiko wanaume na wanawake.
Wachezaji ngoma kutoka Nyasa walialikwa kucheza ngoma za jadi nchi jirani za Msumbiji na Malawi, jambo ambalo hadi sasa bado linadumishwa la watanzania kualikwa kucheza ngoma Msumbiji au wa Msumbiji kualikwa Tanzania hasa vijiji vya mpakani kama vile Chiwindi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.