MKOA wa Ruvuma unatarajia kuzindua kampeni ya kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) Julai 22 mwaka huu katika uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Mwenyekiti wa Kampeni hiyo katika Mkoa wa Ruvuma Ndugu Stephen Ndaki ambaye pia ni Katibu TawalaMkoa wa Ruvuma,amesema mara baada ya uzinduzi wa kitaifa,kampeni hiyo inatarajia kufanyika kwa siku kumi kisha kuendelea hadi Desemba 2023.
Hata hivyo amesema kampeni hiyo inatarajia kufanyika katika Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma ambapo kila Halmashauri kampeni itafanyika katika kata kumi na kwamba katika kila Kata kampeni itafanyika katika vijiji vitatu.
Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Songea mjini Dkt.Damas Ndumbaro ameitaja Kampeni ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kuwa inalenga kulinda na kukuza haki ya upatikanaji haki kupitia huduma za msaada wa kisheria nchini’’,alisisitiza.
“Kampeni inatarajia kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza hususan wanawake,Watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu,kampeni itachangia kuimarisha amani na utulivu na kuleta utengamano wa kitaifa’’,alisisitiza.
Dkt.Ndumbaro amesema kampeni hiyo inatarajia kufanyika kwa miaka mitatu kuanzia Machi 2023 hadi Februari 2026 na kwamba kampeni inafanyika katika nchi nzima kwenye mikoa yote Tanzania bara na Zanzibar kwa kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi.
Amebainisha zaidi kuwa elimu ya kisheria italenga katika masuala ya ukatili wa kijinsia,migogoro ya ardhi,mirathi,usuluhishi kwa njia mbadala,mifumo ya kisheria na masuala yahusuyo haki za binadamu kwa ujumla.
“Ni matarajio yangu kwamba wadau wote wa huduma ya msaada wa sheria nchini watashiriki ipasavyo katika kutekeleza shughuli za kampeni hii ambayo itaboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza na kupunguza matukio ya udhalilishaji wa kijinsia na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini’’,alisisitiza Ndumbaro.
Kumekuwa na ongezeko la wananchi waliopata huduma ya msaada wa kisheria hapa nchini ambapo takwimu za hivi karibuni zinaonesha katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2022,jumla ya watu 41,924 walipatiwa huduma ya msaada wa kisheria kati yao wanaume 17,068 na wanawake 24,856.
Pichani ni Mwenyekiti wa Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ambaye pia ni Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Ndugu Stephen Ndaki
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Juni 12,2023
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.