Wadau wa maliasili katika Mkoa wa Ruvuma wameazimia kuweka vijiji vyote kwenye mpango wa usimamizi jumuishi ili kukabiliana changamoto ya moto.
Maazimio hayo yamepitishwa kwenye kikao cha wadau hao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mipango Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mjini Songea, kilichoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mheshimiwa Peres Magiri.
Kikao hicho kimefadhiliwa na Mradi wa Panda miti kibiashara na kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) mameneja wa mashamba ya miti ya serikali,Mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha SUA na wawezeshaji wa majanga ya moto na usimamizi wa moto vijijini.
Mwezeshaji Andrew Fernand akizungumzia usimamizi wa moto vijijini,amesema mpango huo unatekelezwa katika Halmashauri kumi hapa nchini katika kipindi cha miaka mitano ambapo ameitaja moja ya Halmashauri hizo ni ya Madaba iliyopo mkoani Ruvuma.
Amesema program hiyo katika Halmashauri ya Madaba inatekelezwa katika kijiji cha Wino na kwamba ili kutekeleza mpango huo kila Halmashauri itakuwa na Msimamizi wa masuala ya moto.
Hata hivyo amesema mpango wa kupambana na moto katika Halmashauri ya Madaba unatekelezwa katika vijiji saba na kwamba vijiji vyote vimeweka sheria zinazosaidia kukabiliana na majanga ya moto unatokea hasa katika kipindi cha kiangazi.
Amesema kati ya vijiji saba vinavyotekeleza mpango huo ni Kijiji kimoja tu cha Wino ndicho kina mfuko wa fedha wa kupambana na moto na kwamba vijiji vinne kati ya saba vimenunua vifaa vya kupambana na majanga ya moto.
“Chanzo kikuu cha moto ni wakulima wanapoandaa mashamba yao,wananchi wanatakiwa kubadilika kifkra kuhusu kuandaa mashamba kwa kuchoma moto,elimu inatakiwa kuwa endelevu Pamoja na ununuzi wa vifaa vya kukabiliana na moto’’,alisema.
Naye Mwakilishi wa Meneja Hifadhi ya Misitu Wino Madaba Goffrey Shio amesema shamba hilo limepanda miti Zaidi ya hekta 5000 ya aina mbalimbali na kwamba hifadhi hiyo katika kipindi cha mwaka 2012 hadi 2024 imeweza kuotesha jumla ya miche milioni 8.8.
Hata hivyo amesema wakulima wenye mashamba ya mabondeni uandaa mashamba yao kwa kutumia moto na kwamba moto huo kila mwaka umekuwa unaleta madhara makubwa kwa kuunguza mashamba ya miti ya wananchi ambapo mwaka 2023 zaidi ya hekta 3000 za mashamba ya miti ya wananchi ziliteketea kwa moto.
Akizungumza kwenye kikao hicho Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Ruvuma SF Melenia Nyabwinyo ameomba kuimarisha ushirikiano baina ya Idara ya Zimamoto na wadau wa misitu Pamoja na wananchi kwa kutoa taarifa mapema za matukio ya moto ili kufanya uchunguzi wa moto kwa wakati.
Nyabwinyo ametoa rai kwa TFS na wamiliki wa misitu kuwalipa posho zao kwa wakati wafanyakazi wanaojitolea kulinda mashamba ya miti na misitu yao ili wasiweze kuhujumu kwa kuanzisha moto baada ya kuchelewa kuwalipa maslahi yao.
Akizungumza wakati anafunga kikao hicho Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mheshimiwa Peres Magiri amesisitiza elimu ya kukabiliana na mto iwe endelevu na itolewe kuanzia ngazi ya vijiji.
Amesisitiza kila Kijiji kianzishe Kamati na vikosi vya kukabiliana na matukio ya moto Pamoja na kutoa mafunzo ya mara kwa mara na ununuzi wa vifaa vya kuzimia moto ili kulinda rasmali za misitu.
“Majukumu ya kuanzisha Kamati za moto za vijiji tumekubaliana kuanzia Julai mwaka huu sanjari na kutoa elimu na namna ya kuunda mfuko wa fedha kwa ajili ya vijiji kuhusu suala la moto’’,alisisitiza Magiri.
Ametaka kuwashirikisha wadau kuanzia ngazi kamati za vijiji hadi kwenye Wilaya kwenye mpango jumuishi wa vijiji kukabiliana, kudhibiti na kuzuia majanga ya moto.
Amesisitiza kuwa wadau wa misitu wana kazi kubwa ya kuwaelimisha wananchi vijijini na wadau wote ili wapate taarifa sahihi katika kudhibiti matukio ya moto.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.