MKOA wa Ruvuma umefanikiwa kuboresha huduma za afya ambapo hivi sasa vituo vya kutolea huduma za afya vimeongezeka hadi kufikia 473.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed ofisini kwake mjini Songea wakati wa mapokezi ya Waziri wa Afya Mheshimiwa Jenista Mhagama.
Kanali Abbas amebainisha kuwa vituo hivyo vya kutolea huduma za afya vinajumuisha hospitali 18,vituo vya afya 50,zahanati 341,kliniki 17 na maabara 47.
Ameongeza kuwa huduma za uchunguzi pia zimeimarika ambapo serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imenunua mashine moja ya CT Scan na Digital X ray 11 na kuzisambaza katika vituo vya kutolea huduma za afya ndani ya Mkoa wa Ruvuma.
“Hapo awali huduma za CT Scan zilikuwa hazipatikani ndani ya Mkoa wa Ruvuma na huduma za x ray zilikuwa zinapatikana katika Halmashauri ya Tunduru na hospitali ya Mkoa tu’’,alisisitiza.
Ameongeza kuwa katika eneo la miundombinu ya afya kazi kubwa imefanyika ambapo hadi kufikia mwaka 2023/2024 shilingi bilioni 32.26 zimetolewa na kwamba katika kipindi hicho hospitali sita za halmashauri zimejengwa ambapo hadi sasa ujenzi wa hospitali hizo umegharimu shilingi bilioni 16.5 na kwamba serikali imetumia shilingi bilioni 1.8 kukarabati hospitali kongwe.
Akizungumzia mradi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa ,Kanali Abbas amesema mradi huo ni mafanikio makubwa ambapo baadhi ya huduma zimeanza kutolewa kwa baadhi ya majengo yaliyokamilika yakiwemo jengo la mionzi lilijengwa kwa shilingi bilioni 2.34.
Majengo mengine ambayo yamekamilika ameyataja kuwa ni jengo la magonjwa ya dharura EMD lililogharimu shilingi milioni 784,ukarabati wa jengo la wagonjwa mahututi (ICU) kwa gharama ya shilingi milioni 152,jengo la tiba mtandao lililogharimu shilingi milioni 33.1.
Hata hivyo amesema ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje OPD unaendelea ambapo hadi sasa shilingi bilioni 3.36 zimetumika,pia serikali imetoa shilingi milioni 650 kwa ajili ya ujenzi wa mtambo wa kuzalisha hewa ya Oksijen na ujenzi wa jengo la huduma ya dialysis unaendelea ambapo jumla ya shilingi milioni 480 zimetolewa na ujenzi umefikia asilimia 78.
Mafanikio mengine ambayo yamepatikana ni katika utoaji wa huduma za afya ya uzazi,mama na mtoto ameyataja kuwa ni wajawazito wanaohudhuria kiliniki wameongezeka na idadi ya wajawazito waliojifungua katika vituo vya afya imeongezeka kutoka asilimia 85 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 99.2 mwaka 2024.
Akizungumza baada ya kupata taarifa hiyo,Waziri wa Afya Mheshimiwa Jenista Mhagama amesema serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya hivyo kufanikisha kutoka huduma za kibingwa katika hospitali zilizopo ndani ya Mkoa.
Amesema serikali imeweka sheria ya Bima ya afya kwa wote ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya afya na kwamba serikali imeshaleta fedha nyingine kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje OPD katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma.
Katika hatua nyingine Waziri Mhagama amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais -TAMISEMI itatoa mafunzo rasmi ya kuwajengea uwezo watoa huduma za Afya ngazi ya jamii 11,515 kuanzia Septemba 30, 2024 ili kufanikisha azma ya Mpango Jumuishi wa wahudumu hao na kuendeleza afua jumuishi za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii.
Waziri Mhagama amesema mpango huo utaanza kwenye Halmashauri 21 ndani ya mikoa 11 katika awamu ya kwanza
“Mikoa ambayo itafikiwa na huduma hii kwa Awamu ya kwanza ni pamoja na Geita, Pwani, Tanga, Songwe, Mbeya, Lindi, Tabora, Kagera, Njombe, Ruvuma, na Kigoma" ameainisha waziri Mhagama na kuongeza kuwa
Ameutaja mpango huo umelenga na unahitaji kuwa na wahudumu wawili wa jinsia ke na me kila mtaa na kila kitongoji,na kwamba uchaguzi wa wahudumu hao umeshirikisha wananchi na wana jamii kutoka kitongoji husika au mtaa husika
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.