WADAU wa Maendeleo ya elimu mkoani Ruvuma wameazimia kufanya vikao na wadau wa elimu kwa kila Halmashauri ambao wanaweza kutoa ahadi ya kuchangia maendeleo katika sekta ya elimu.
Azimio hilo limetolewa katika kikao cha wadau wa maendeleo ya elimu Mkoa wa Ruvuma kilichohusu kujadili namna ya kunufaika kupitia Mfuko wa kusaidia maendeleo ya elimu Duniani (GPE) ambacho kimefanyika kwa siku moja kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Mgeni rasmi katika kikao hicho alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Kapenjama Ndile.
Akizungumza kwenye kikao hicho,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri zote nane kuhakikisha wanafanya vikao vya kukutana na wadau wa maendeleo ya elimu na kuleta taarifa za vikao hivyo Pamoja na orodha ya wadau na kiwango cha fedha na vifaa ambavyo wameahidi kusaidia sekta ya elimu katika Halmashauri husika.
“Taarifa hiyo ifike katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kabla ya Agosti 15 mwaka huu na ofisi ya Mkuu wa Mkoa itajaza taarifa zinazohitajika kiserikali na kuwasilisha Wizara ya Elimu kabla ya Agosti 25,2023 ili Mkoa wa Ruvuma uwe sehemu ya watanzania watakaonufaika na mradi wa GPE’’,alisisitiza Mkuu wa Mkoa.
Akizungumzia mfuko wa GPE kwenye kikao hicho,Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Stephen Ndaki amesema Tanzania ilianza kunufaika na mfuko wa GPE tangu mwaka 2013 na kwamba hadi sasa serikali imenufaika kwa awamu mbili.
Amesema awamu ya kwanza ya unufaikaji wa mfuko huo ilianza mwaka 2014 hadi 2018 na awamu ya pili ilianza mwaka 2019 na inatarajia kufikia ukomo Januari 2024.
Hata hivyo amesema katika ufadhili unaotarajia kuanza mwaka wa fedha 2023/2024,Tanzania imepewa nafasi ya kuomba fedha kupitia aina tatu za ufadhili ambazo amezitaja kuwa ni System capacity Grant (SCG),Sysytem transformation grant (STG) na multilier grant (MG).
“Ndugu wadau wa elimu,mpaka sasa kupitia idhini ya Bodi ya wakurugenzi wa GPE,nchi imenufaika kupitia SCG imepata Dola za Marekani 3,999,000 na kupitia STG nchi imepata Dola za Marekani 84,664,800’’,alisema Ndaki.
Hata hivyo amebainisha kuwa maombi yaliyowasilishwa ili nchi iweze kupata fedha za ufadhili kupitia MG hayajafanikiwa kufikia hatua ya kupata idhini ya Bodi ya wakurugenzi wa GPE.
Amesisitiza kuwa ili kupata fedha ambazo zimefungiwa inahitajika wadau wa elimu kutoa ahadi au mali kauli kuonesha namna gani wapo tayari kuchangia maendeleo ya elimu nchini na kwamba kiasi cha fedha ambacho kitachangiwa kitabaki ndani ya Mkoa kwa ajili ya maendeleo ya elimu.
Akitoa mada ya Mfuko wa kusaidia maendeleo ya elimu Duniani (GPE) kwenye kikao hicho,Mwezeshaji Mathias Tilia amevitaja vigezo vinavyotumika ili nchi iweze kupata ufadhili kupitia mfumo wa MG kuwa ni kila Dola tatu za Marekani zitakazotolewa na wadau wa maendeleo wa nje,GPE itatoa Dola moja ya Marekani.
Ameongeza kuwa kila Dola moja ya Marekani itakayotolewa na wadau wa maendeleo ya elimu nchini,GPE itaoa Dola moja ya Marekani.
Amesema Wizara ya elimu imekusudia kuandaa hafla ya kuhamasisha wadau wa elimu nchini ili waweze kufadhili na kuongeza ufadhili kwenye masuala ya elimu msingi na kwamba fedha hizo zitachangia kuiwezesha serikali kutekeleza mipango mipya iliyoibuliwa sanjari na mabadiliko ya Sera na mitaala ya elimu ili kutekeleza eneo la mafunzo ya amali
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.