Maandalizi ya Tamasha la Tatu la Utamaduni Kitaifa, linalotarajiwa kufanyika kwa siku nne kuanzia Septemba 20 hadi 23, 2024, wilayani Songea mkoani Ruvuma, yanaendelea kuungwa mkono na wafanyabiashara, taasisi, na mashirika mbalimbali.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa,Songea Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amewasihi wafanyabiashara na viongozi wa taasisi hizo kuendelea kushirikiana naye ili kufanikisha Tamasha na mapokezi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye atakuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo.
"Kila jambo linawezekana, tuendelee kuwa wamoja, tushirikiane kuyafanikisha yote yanayotuhusu na kuchangamkia fursa hizi. Naomba ushirikiano wenu wa hali na mali," alisisitiza Kanali Ahmed.
Amebainisha kuwa baada ya Rais kuhudhuria tamasha hilo, atafanya ziara katika wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma, pamoja na kushiriki Mkutano wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na kuzungumza na wakazi wa Ruvuma katika uwanja wa Majimaji, tarehe 28 Septemba 2024.
Naye Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Mkoa wa Ruvuma, Izack Mwilamba, amesisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kushirikiana na Mkuu wa Mkoa, akilitaja tamasha hilo kama fursa muhimu kwa uchumi wa wafanyabiashara wa Mkoa wa Ruvuma.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma, Komredi Oddo Mwisho, amewaomba wafanyabiashara kuendelea kujitolea kusaidia maandalizi ya tamasha hilo na kumpokea Rais kwa namna ya kipekee atakapowasili katika Mkoa wa Ruvuma
Tamasha hili la Utamaduni la tatu Kitaifa linatarajiwa kuvutia wageni kutoka sehemu mbalimbali nchini, na hivyo kuleta fursa za kibiashara kwa wakazi wa Ruvuma.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.