WAFANYAKAZI wa Mkoa wa Ruvuma wameiomba Serikali kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu changamoto zao za kiutumishi.
Ombi hilo llimetolewa katika risala ya watumishi hao iliyosomwa na Mratibu wa Chama cha TUCTA Ashirafu Chussi katika maadhimisho ya Mei Mosi yaliyofanyika kimkoa Wilaya ya Namtumbo.
Risala hiyo imezitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili watumishi kuwa ni mishahara ya watumishi bado ni midogo ukilinganisha na gharama za maisha hivyo wameiomba Serikali kuongeza mishahara na kuboresha maslai ya watumishi.
‘’Tunaiomba Serikali kupitia Mei Mosi hii kwa jicho la pekee kabisa iongoze mishahara na kuboresha maslahi kwa wafanyakazi kwa muda mrefu mishahara haijaongozwa takribani miaka sita sasa’’, imeeleza risala hiyo.
Watumishi hao wamesema kutoongeza mishahara kwa muda mrefu kunashusha morali ya utendaji kazi kwa wafanyakazi na kusababisha kutoa huduma duni kwa jamii.
Kulingana na risala hiyo changamoto nyingine zinazowakabili watumishi wa Mkoa wa Ruvuma ni baadhi ya watumishi kutolipwa madeni kwa wakati na baadhi ya waajiri kutolipa nauli za watumishi na mizigo yao pindi wanapostaafu.
Changamoto nyingine wamezitaja kuwa ni baadhi ya waajiri kuendelea kufanya kikao kimoja tu cha Baraza la wafanyakazi ili kupitisha bajeti na wengi wao kutolipa stahiki sahihi za wajumbe kwa mujibu wa muongozo kwa mfano 2022 kati ya Halmashauri nane za Mkoa wa Ruvuma ni Halmashauri moja tu ya Manispaa ndio imelipa.
Kwa mujibu wa risala hiyo baadhi ya waajiri kutopeleka michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa wakati na kusababisha baadhi ya watumishi kutolipwa stahiki zao za mafao kwa wakati na baadhi ya watumishi kufanyishwa kazi siku za mapumziko bila kulipwa stahiki zao za saa za ziada.
Hata hivyo uwepo muongozo mpya kandamizi wa upandishaji wa madaraja ya mishahara unaotaka mtumishi wa ajira mpya kukaa miaka mitano na miaka minne kwa aliyopo kazini ili kupata sifa ya kupandishwa daraja ni changamoto kubwa kwa wafanyakazi wetu.
Licha ya changamoto hizo wafanyakazi wa Mkoa wa Ruvuma wameahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi kwa maslahi mapana ya Nchi yetu na Mkoa huku wakiamini Serikali itachukua hatua kwa wakati kutatua changamoto hizo.
Akijibu risala hiyo mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Dkt Julius Ningu ameahidi Serikali kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu changamoto hizo.
Hata hivyo RC Ibuge ametoa rai kwa waajiri kuhakikisha wanajitahidi kuzingatia maslahi kwa watumishi na kulipa madeni kwa wakati sanjari na kuandaa nauli za watumishi na mizigo yao kuandaliwa kwa wakati.
‘’Natoa maelekeza kwa waajiri wote kuhakikisha wanazingatia muongozo uliowekwa na Serikali katika kushughulikia stahiki za watumishi na kupeleka michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii’’, amesema RC Ibuge.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya Mei Mosi 2022 ni mishahara na maslaHi bora kwa wafanyakazi ndio kilio chetu.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Mei 2,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.