HOSPITALI ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo shirika lisilo la kiserikali la MDH,imeanza kutoa elimu na upimaji wa ugonjwa wa kifua kikuu kwa jamii ya wafugaji katika maeneo wanayoishi.
Hatua hiyo inatokana na kundi hilo kubwa, kuwa miongoni mwa makundi yaliyopo hatarini kupata maambukizi ya ugonjwa huo unaotajwa kupoteza maisha ya watu wengi Duniani hasa katika nchi za kusini mwa Bara la Afrika.
Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema,jamii ya wafugaji iko kwenye hatari ya kupata ugonjwa huo kutokana na maisha wanayoishi hasa unywaji wa maziwa ya ng’ombe yasiyochenshwa vizuri.
Alisema,unywaji wa maziwa ya ng’ombe holela ni hatari kwani yana vimelea ambavyo ni chanzo kikubwa cha kuenea kwa ugonjwa wa kifua kikuu na kuitaka jamii kuepuka kunywa maziwa yasiyochemshwa,badala yake watumie maziwa yaliyochemshwa ambayo ni salama na hayana madhara kwa binadamu.
Alisema,wilaya ya Tunduru inatajwa kuwa miongoni mwa wilaya zenye maambukizi makubwa ya kifua kikuu hapa nchini,na sababu mojawapo ya kuongeza kwa ugonjwa huo ni unywaji holela wa maziwa ya ng’ombe wasiopimwa afya zao.
Kihongole alitaja makundi yaliyo katika hatari ya kupata maradhi hayo ni wazee,kwani binadamu kadri umri unavyokuwa mkubwa kinga za mwili zinapungua na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Kwa mujibu wa Kihongole,makundi mengine ni wasafiri,watu wanaoishi katika msongamano wakiwemo wafungwa,wanafunzi na wanaoishi kwenye nyumba ambazo hazina hewa au mwanga wa kutosha.
Ametaja dalili za mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo ni kukohoa kwa wiki mbili au zaidi,kutokwa na jasho jingi hasa nyakati za usiku,kupungua uzito,kupoteza hamu ya kula na kwa watoto kulia lia, kuwa na homa za mara kwa mara na kuchelewa kukua.
Kwa upande wake Afisa mipango wa shirika la MDH mkoani Ruvuma Dkt Hellen Mwita,ameikumbusha jamii kuwa na utaratibu wa kwenda katika vituo vya kutolea huduma kwa ajili ya uchunguzi wa afya za mara kwa mara.
Dr Mwita ametoa wito kwa akina mama,pindi wanapoona dalili za ujauzito ni vema kwenda kliniki mapema ili kupata ushauri wa wataalam na wanatumia zahanati na vituo vya afya vilivyopo kujifungulia,badala ya kubaki nyumbani kwani ni hatari kwa afya zao na watoto wakati wa kujifungua.
Diwani wa kata ya Misechela Zuberi Diwani,amewataka wafugaji kubadilika na kuanza kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kuhudhuria kampeni za uchunguzi wa afya zinazoendeshwa na wataalam wa wizara ya afya na wadau wengine.
Ameishukuru serikali kupitia Hospitali ya wilaya ya Tunduru kitengo cha kifua kikuu na ukoma,kwenda kufanya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu kwa jamii ya wafugaji ambayo kwa muda mrefu haiwajawahi kufikiwa na huduma zozote za afya kwenye maeneo yao.
Laisi Maduka mfugaji,ameiomba serikali kupeleka huduma hizo mara kwa mara kwenye maeneo yao ili waweze kupata matibabu,kwa kuwa wengi wao wanaishi mbali na maeneo ya kutolea huduma za afya.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.