WAKANDARASI wazawa wanaotekeleza miradi ya ujenzi wa barabara mkoani Ruvuma, wamemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na serikali yake ya awamu ya sita kwa kuwaamini na kuwapatia miradi mingi iliyowajengea uwezo zaidi na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.
Aidha,wamempongeza Rais Samia kuipatia fedha za kutosha,wakala wa barabara za vijijini na mijini(Tarura) zilizowezesha wakandarasi wazawa kupata kazi,hali ambayo imewasaidia kupata kipato cha kuhudumia familia na kuchangia maendeleo ya mkoa huo.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake Valence Urio amesema,katika kipindi cha miaka miwili cha Rais Dkt Samia kumekuwa na mafanikio makubwa kwani miradi mingi ya barabara za vijijini na mijini zimetekelezwa na wakandarasi wazawa.
Urio ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Ovans Construction Ltd amesema,kabla ya serikali ya awamu ya sita kuingia madarakani changamoto kubwa ilikuwa miradi mingi inayotangazwa,michache ndiyo iliyotekelezwa tofauti na awamu ya sita ambapo miradi inayotangwa inatekelezwa na wanapewa wakandarasi wa ndani(wazawa).
Amesema kutokana na mageuzi makubwa yaliyofanywa na serikali kwenye sekta ya Barabara, imewafanya wakandarasi kutosheka na kubaki katika mkoa mmoja au miwili tu, badala ya kuzurura kwenda mikoa mingine kutafuta kazi.
“Namshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuturejeshea fursa hii ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati,miaka ya nyuma tumepitia wakati mgumu kwani kazi nyingi za ujenzi wa miradi ya barabara walipewa wakandarasi wakubwa hasa kutoka nje.”alisema Urio.
Pia amefurahishwa na uamuzi wa Rais Dkt Samia,kuwapunguzia tozo ikiwemo kulipia galantii kwenye miradi yote,lakini kutokana na maboresho ya sheria iliyofanywa na serikali ya awamu ya sita kuondoa utaratibu huo sasa mkandarasi analipia shilingi bilioni moja tu kwenye kazi zote.
Urio,ameiomba serikali kuendelea kuwaamini wakandarasi wa ndani na kuwapa kazi za ujenzi wa miradi mikubwa ya maendeleo kwani sasa wana uzoefu wa kutosha na uwezo mkubwa.
Amewaasa wakandarasi wenzake kubadilika,kufanya kazi kwa weledi,uaminifu na kufanya kazi zenye ubora ili kurudisha imani kwa serikali na waweze kushindana na wakandarasi wa nje.
Kwa upande wake Meneja wa TARURA wilayani Mbinga Oscar Mussa amesema,katika miaka miwili ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita wamefanikiwa kufungua barabara mpya zenye urefu wa kilomita 500,kujenga madaraja na makalavati 106 na kujenga barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 5.67.
Ameishukuru Serikali kuiongezea fedha Tarura wilaya ya Mbinga ambapo mwaka wa fedha 2021/2022 walipokea jumla ya shilingi bilioni 4.5 ambazo zimewezesha kufanya matengeneza barabara zenye urefu kilomita 287.77 kujenga barabara kwa kiwango cha lami urefu wa kilomita 2.17 na kujenga madaraja makubwa na madogo 53.
Amesema,kwa mwaka wa fedha 2022/2023 wametengewa shilingi bilioni 5.8 kutoka bilioni 4.5 za mwaka uliopita,na fedha hizo zimetumika kujenga barabara kwa kiwango cha lami kilomita 3.5,kufungua na kufanya matengenezo ya barabara kilomita 217,kujenga madaraja makubwa na madogo na makalavati 53 na kufunga taa za barabarani 30 katika wilaya yote ya Mbinga.
Amewataka wananchi na watumiaji wa barabara hizo,kujiepusha na uharibifu wa miundombinu ya barabara kwa kutozidisha uzito wa magari,kufanya shughuli za kibinadamu kando kando ya barabara na kuacha kupitisha mitaro ya maji ili barabara hizo ziweze kudumu kwa muda mrefu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.