MRADI wa maji unaotekelezwa katika vijiji vinne vya Mtepa,Kipingo,LItuta na Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 na tayari wananchi wa kijiji cha Kipingo wameanza kupata maji.
Meneja wa Mamlaka ya Maji vijijini RUWASA Wilaya ya Songea Mhandisi Mathias Charles amesema mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.3 ambapo matanki mawili yamejengwa,huku tanki moja la Kipingo limejazwa maji kwa ajili ya kuanza kuhudumia wananchi.
Hata hivyo amesema ili kukamilisha tanki moja la Madaba pachani zinasubiriwa pampu za kusukumia maji ambazo zitafungwa wakati wowote kuanzia sasa na kwamba mradi huo ni mkubwa umehusisha ujenzi wa matanki mawili na ulazaji wa mabomba kilometa 34.
“Wananchi wa kipingo wameanza kupata maji,tunatarajia maeneo mengine yaliyobakia kati ya Januari 18 hadi 25 mwaka huu,wananchi wataanza kupata huduma ya maji,tunamshukuru mheshimiwa Rais kwa kutupatia fedha zilizotekeleza mradi huu hivyo kuondoa kero ya maji kwa wananchi’’,alisema Charles.
Olaph Pilli ni Diwani wa Kata ya Lituta Halmashauri ya Madaba,amesema kabla ya kutekeleza mradi huu,Madaba ilikuwa na changamoto kubwa ya maji ambapo amesema mradi huu wa maji umekuwa mkombozi mkubwa katika kata yake.
“Hali ya maji katika Halmashauri yetu ya Madaba hasa katika Kata ya Lituta ilikuwa ni tete,wananchi walikuwa wanapata shida ya maji,lakini baada ya mradi huu sasa Madaba haitakuwa na shida tena ya maji,tuna maji ya kutosha’’,alisisitiza Diwani Pilli.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya watumiaji maji vijiji vinne vya Mtepa,Kipingo,Lituta na Madaba Modestus Mgina ameipongeza RUWASA kwa kukamilisha ujenzi wa mradi huo ambapo tayari tanki moja la Kipingo limejazwa maji tayari kwa kuanza kusambazwa kwa wananchi.
Amesema mradi huo unakwenda kuwanufaisha wananchi zaidi ya 19,000 ambapo ameitaja hali ya maji kabla ya kutekeleza mradi huu ilikuwa ni mbaya,wananchi walikuwa wanapata maji ya mgawo kati ya siku tatu hadi tano.
“Maji yalikuwa yanapatikana kwa vurugu na ugomvi mkubwa,ilikuwa ni vita ya maji,lakini sasa mradi huu unamaliza kero hiyo,tunamshukuru sana Rais Dkt.John Magufuli,tuna raha sana kupata mradi huu’’,,alisema.
Desderia Ngatunga ni Mkazi wa Madaba akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Madaba, amesema wanaishukuru serikali kwa kuwapatia mradi mkubwa wa maji ambapo sasa Madaba itaneemeka kwa maji mengi ya kutosha na kumaliza kilio cha maji cha miaka mingi.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Januari 18,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.