Wakulima wa Songea wagomea bei mnada wa soya
Waingiza milioni 400 katika ufuta
MNADA wa nane wa mazao ya ufuta na soya ulioshirikisha Halmashauri tano za Mkoa wa Ruvuma na vyama vya msingi vya ushirika 11 umewawezesha wakulima kuuza kilo zaidi ya 264,000 za ufuta na kuwaingizia zaidi ya milioni 400.
Akizungumza mara baada ya kufanyika mnada huo katika soko la mazao la Lilambo,Meneja Operesheni wa Chama Kikuu cha Ushirika wa mazao ya kilimo Songea na Namtumbo (SONAMCU) Zamakanary Komba amezitaja Halmashauri tano zilizoshiriki katika mnada wa zao la ufuta kuwa ni Halmashauri ya Mbinga, Halmashauri ya Songea,Madaba na Nyasa.
Amevitaja vyama 11 vilivyoshiriki katika mnada huo kuwa ni Kingambi,Tingi,Kilumba,Mpiki,Lina,MugisoNalisi,Songea West, Amkeni, Muungano na Tama na kwamba katika kilo za ufuta zilizouzwa katika mnada huo,bei ya juu iliyokubalika na wakulima ilikuwa ni sh.1930 na baada ya kutoa tozo mkulima anauza kwa sh.1759.
“Pesa ambayo imekwenda moja kwa moja kwa wakulima katika mnada wa leo ni shilingi milioni 465,250,223,lakini kabla ya makato kwenda kwa wakulima,fedha ilikuwa ni zaidi ya milioni 510’’,alisisitiza Komba.
Komba amesema kupitia mnada huo, tozo ya mfuko wa maendeleo katika Halmashauri imepatikana shilingi milioni 7.9 na kwamba ushuru wa Halmashauri ni zaidi ya sh. Milioni 20.6.
Hata hivyo katika mnada wa zao la soya ambao umeshirikisha Halmashauri mbili wakulima wamegomea bei ya zao hilo ambayo bei ya juu ilikuwa ni 680 kwa kilo ambapo ukitoa tozo mkulima alikuwa anabakiwa na sh.558.
“Wakulima wa soya wamegomea bei hiyo kwa hiyo tumeusogeza mbele mnada huo hadi Jumatatu ijayo,leo tuliangalia asubuhi bei ya Dar es salaam ilikuwa kilo ni sh.800,Morogoro sh.850 kwa hiyo tunawashauri wenye Kampuni wanunue bei nzuri kutoka kwa wakulima’’,alisisitiza Komba.
Wakulima wa zao la ufuta katika Wilaya za Namtumbo,Songea na Tunduru mkoani Ruvuma wameanza kunufaika na zao hilo baada ya kupokea shilingi bilioni 16.8 tangu kuanza kuuza zao hilo kwa mfumo wa stakabadhi ghalani Apirili 30 mwaka huu
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Juni 15,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.