WAKULIMA wa zao la korosho katika kijiji cha Mtonya kata ya Mindu wilayani Tunduru,wamemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutoa bure pembejeo na dawa(Sulphar) za kupulizia mashamba ya korosho.
Wamesema,mpango huo uliofanywa na Rais Samia umesaidia kuhamasisha wakulima wengi kufufua mashamba yao na kueleza kuwa utaongeza uzalishaji wa korosho hapa wilayani Tunduru.
Stamili Yakiti,ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa uamuzi wa kuweka ruzuku kwenye pembejeo za korosho kwa kuwa utachochea na kuongeza uzalishaji.
Alisema,miaka ya karibuni uzalishaji wa zao hilo ulishuka kutokana na wafanyabiashara binafsi kuuza pembejeo kwa bei kubwa hali iliyosababisha baadhi ya wakulima kushindwa kuhudumia mashamba yao.
Joseph Kalo mkulima kutoka kijiji cha Liwangula alisema,uamuzi wa Rais Samia ni mzuri na unakwenda kuleta tija kwa wakulima tofauti na miaka ya nyuma ambapo pembejeo zilizoletwa na wafanyabiashara zilikuwa chache na ziliuzwa kwa bei kubwa,hivyo kusababisha baadhi ya wakulima kutelekeza mashamba yao.
Alisema,hata mfumo wa ugawaji wa pembejeo mwaka huu ni mzuri kwani hautoi nafasi kwa wasimamizi kuiba na wakulima wanapata pembejeo kulingana na ukubwa wa mashamba na mahitaji yao.
Hata hivyo,ameiomba serikali kuongeza kiwango cha dawa hasa Sulphar ya maji ili kukidhi mahitaji hatua itakayosaidia kuongeza uzalishaji wa korosho mashambani kwa msimu wa kilimo 2023/2024.
Meneja wa Chama kikuu cha ushirika wilaya ya Tunduru(Tamcu Ltd)Iman Kalembo alisema,utaratibu uliotumika mwaka huu ni nzuri na wakulima wengi wana ufurahia na hadi sasa hakuna malalamiko yaliyojitokeza ambapo amemshukuru Rais Dkt Samia kwa kuwezesha upatikanaji wa pembejeo.
Amewashauri wakulima wa korosho kuwa,baada ya kukamilika kwa zoezi hilo kuwashirikisha maafisa ugani kwa ajili ya kufanya tathimini ya ukubwa wa mashamba yao ili waweze kupata mahitaji halisi ya pembejeo.
Alisema,makisio ya uzalishaji wa korosho katika msimu wa mwaka 2023/2024 ni tani 25,000 hata hivyo uzalishaji unaweza kuongezeka kutokana na mwitikio mkubwa wa wakulima kuchukua pembejeo zilizotolewa bure na serikali zitaongeza uzalishaji wa zao hilo.
Kalembo alisema,lengo la serikali ya awamu ya sita ni kuhamasisha matumizi ya dawa ili kukabiliana na magonjwa ya korosho na hivyo kuwafanya wakulima kubadilisha maisha yao kupitia zao hilo.
Amewataka wakulima kutumia dawa hizo kwa usahihi na kufuata maelekezo ya wataalam ili kuzalisha kwa wingi,kukuza uchumi na hatimaye waweze kujikomboa na umaskini kupitia shughuli zao za kilimo cha korosho.
Meneja wa bodi ya korosho Tanzania tawi la Tunduru Shauri Mokiwa amewataka wakulima kutambua kuwa,ruzuku ya pembejeo ya zao la korosho inayotolewa na serikali ni mchango wake katika kumpunguzia mkulima gharama ya uzalishaji wa zao hilo.
Alisema,serikali inachangia kwa sehemu ndogo hivyo ni muhimu kwa wakulima kujiwekea akiba ya fedha kwa ajili ya kuongeza kununua viuatilifu kwa wafanyabiashara ili waweze kutosheleza mahitaji yao.
Afisa kilimo wa kata ya Mindu Agrey Fungo alisema,mwitikio wa wakulima kuchukua pembejeo ni mkubwa na hakuna changamoto iliyotokea kutokana na utaratibu mzuri uliowekwa ambao umehamasisha wakulima wengi kufufua mashamba yao.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.