Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amewataka wakuu wa Taasisi za Serikali kusimamia miradi ya maendeleo kwa umakini na kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati ili iweze kutoa huduma kwa wananchi.
Kanali Thomas ametoa maagizo hayo wakati anazungumza katika kikao na wakuu wa Taasisi za serikali mkoani Ruvuma kilichofanyika katika ukumbi wa Mipango uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
Amesema Serikali imekuwa inatoa pesa nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali ikiwemo barabara, Maji na Umeme ili wananchi waweze kunufaika na kazi inayofanywa na serikali kwa kupewa huduma bora.
“Tumekuwa mashahidi kila sekta inapewa pesa nyingi na Mh. Rais Dkt.samia Suluhu Hassan hivyo ni jukumu la kila Mkuu wa Taasisi kusimamia kikamilifu miradi hiyo “‘ alisema RC Thomas.
Kanali Thomasi amewasisitiza watendaji hao kuwa na umoja,mshikamano,kujitambua na kushirikiana na watumishi wanaowasimamia ili miradi hiyo iweze kutekelezwa kwa ufanisi na tija.
Katika kikao hicho Kanali Thomas amewaomba wakuu wa Taasisi kuwa na utamaduni wa kupanda miti ya matunda ambayo wataitumia kama chakula ili waweze kupambana na tatizo la udumavu katika Mkoa.
Naye, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Roman Mbukwini amesema wamejipanga kukagua barabara sehemu zilizoharibika na hatarishi na kuzifanyia marekebisho.
Akizungumza kwenye kikao hicho,Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi Songea (SOUWASA) Mhandisi Patrick Kibasa amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi wasiendelee na shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji ili wananchi wa mji wa Songea waendelee kupata maji safi na salama.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.