WALIMU 24 na wanafunzi sita kutoka sekondari ya Mwanakwereke C Zanzibar wapo mkoani Ruvuma kwa ziara ya siku kumi ya mafunzo na kutembelea vivutio vya utalii.
Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Pololet Mgema amesema ziara hiyo inaanza Desemba 8 hadi Desemba 16 mwaka huu.
Amesema walimu na wanafunzi hao wakiwa wilayani Songea Desemba 8 watashiriki zoezi la usafi katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma,ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Tanganyika.
“Desemba 9,walimu na wanafunzi watashiriki mdahalo wa kuadhimisha miaka 61 ya Uhuru wa Tanganyika kwenye ukumbi wa Songea klabu’’,alisema.
Amesema kuanzia Desemba 10 hadi 13,walimu na wanafunzi hao wataanza kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo mjini Songea,vikiwemo mlima Matogoro ili kuangalia chanzo cha Mto Ruvuma,Makumbusho ya Taifa ya Majimaji,Hifadhi ya asili ya Luhira,Makumbusho ya Rashid Kawawa na mapango ya Nduna Songea Mbano katika mlima Chandamali.
Kulingana na ratiba ya ziara hiyo, Desemba 14 walimu na wanafunzi hao watembelea Lugari Zoo iliyopo mjini Mbinga na vivutio mbalimbali vilivyopo katika ziwa Nyasa wilaya ya Nyasa.
Amesema Desemba 15,watatembelea na kujifunza masuala mbalimbali kwenye Taasisi zilizopo katika Manispaa ya Songea na Desemba 16,watahitimisha ziara yao kwa kukutana na Jumuiya ya wakufunzi na wafanyakazi wa Chuo cha Ualimu Songea.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
Desemba 7,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.