WANAFUNZI wa shule ya Sekondari Makita Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma,wameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea vyumba viwili vya madarasa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema,mradi huo wa umewaondolea adha ya kubanana katika kichumba kimoja na vitawapa fursa ya kukaa kwa nafasi na kuwaongezea morali ya kusoma kwa bidii.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake John Kapinga alieleza kuwa,ujenzi wa madarasa hayo yatakuwa chachu katika safari yao ya masomo, kwa kuwa walimu nao watapata nafasi kubwa ya kuwafundisha na wao kuwaongezea umaskini wa kusikiliza wanachofundishwa darasani.
Mkuu wa shule hiyo Emmanuel Mwamasika alisema,shule hiyo ilipokea kiasi cha Sh.milioni 40 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa.
Alisema,kati ya fedha hizo Sh.milioni 31,493,400.00 zimetumika kununua vifaa vya ujenzi,Sh.milioni 5,841,600.00 zimetumika kulipa gharama ya ufundi na Sh.milioni 2,665,000.00 kutengeneza viti na meza 41.
Mwamasika alieleza kuwa,Halmashauri ya Mji Mbinga imechangia jumla ya Sh.milioni 2,535,000.00 kwa ajili ya kuongeza viti na meza 39 na wananchi wamechangia nguvu kazi kwa kuleta kokoto zinazokadiriwa kuwa na gharama ya Sh.600,000.
Mwamasika alisema, baada ya kukamilika mradi huo umesaidia kuondoa uhaba wa vyumba vya madarasa na kupunguza msongamano kwa wanafunzi darasani,wanafunzi kukaa katika mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia na kuinua taaluma kwa kuwa wanafunzi watasoma katika mazingira mazuri.
Aidha alisema,vyumba hivyo vitatoa fursa kwa wanafunzi kupata elimu itakayowasaidia katika mapambano dhidi ya Rushwa,maralia,lishe duni,kuimarisha usawa na hata kutokomeza ukatili wa kijinsia na unyanyapaa.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 Abdalla Shaibu Kaim,ameipongeza Halmashauri ya mji Mbinga kwa usimamizi wa mradi huo ambao umewasaidia sana wanafunzi kuondokana na changamoto ya kukaa wengi katika chumba kimoja.
Amewaasa watumiaji wa majengo hayo wanafunzi na walimu,kuhakikisha wanatunza majengo hayo ili yaweze kuwasaidia kupata elimu bora ambayo itawasaidia kupambana na changamoto mbalimbali na kutimiza malengo yao.
Amemtaka Mhandisi wa ujenzi wa Halmashauari hiyo kuhakikisha anatumia weledi katika majukumu yake na kutanguliza uzalendo mbele, badala ya kufanya kazi kwa kulipua kwa sababu serikali inaingia gharama kubwa katika kutekeleza miradi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.