Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imeanza kuvuna matunda ya juhudi zake katika kuboresha lishe kwa wanafunzi shuleni, hatua inayochochea ongezeko la ufaulu wa wanafunzi.
Kwa mujibu wa taarifa ya karibuni, asilimia ya wanafunzi wanaopata chakula shuleni imeongezeka kutoka asilimia 67 hadi 77 ndani ya mwaka mmoja.
Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Kapenjama Ndile, amesema mafanikio hayo ni matokeo ya utekelezaji wa mkataba wa lishe unaopitiwa kila baada ya miezi mitatu. Ametaja kuwa lishe bora shuleni ni msingi muhimu wa kuinua kiwango cha elimu kwa watoto.
Hata hivyo Afisa Lishe wa Manispaa, Albert Sinkamba, amesema bado kuna kazi kubwa ya kufanya kwani udumavu kwa watoto unachangiwa na upungufu wa virutubisho muhimu.
Amebainisha kuwa juhudi zinaelekezwa katika kuelimisha jamii kupitia siku za afya na kuhakikisha wajawazito wanapata huduma bora za lishe mapema.
Katika kuhamasisha utekelezaji wa lishe shuleni, Manispaa ya Songea imeanzisha zawadi kwa kata zinazofanya vizuri.
Kata ya Subira imeibuka kidedea kwa kutoa chakula kwa asilimia 97 ya wanafunzi wake, na Mtendaji wake, Ndugu Alex Kapinga, kupongezwa kwa zawadi ya cheti na shilingi 100,000.
Kapinga amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa walimu na wazazi waliolima mashamba ya shule kwa ajili ya chakula cha wanafunzi. Amehimiza kata nyingine kuiga mfano huo ili kuhakikisha kila mtoto anapata lishe bora akiwa shuleni.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.