Wakazi wapatao 11,080 kutoka vijiji vya Ngumbo, Mbuli, Mkili, Liwundi na Yola wilayani Nyasa mkoani Ruvuma wanatarajiwa kupata huduma ya maji safi na salama kupitia mradi wa maji wa Ngumbo Group awamu ya pili.
Hatua hii itawezesha wananchi kutumia muda mwingi kwenye shughuli za kiuchumi na kupunguza magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Nyasa, Mhandisi Evath Rwekaza, amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 75.
“Tayari baadhi ya wananchi wameanza kupata huduma kupitia vituo vya maji vilivyojengwa na maunganisho binafsi”,alisema Rwekaza.
Naye Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhandisi Stella Martin Manyanya, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo, amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi bila kujali hali zao za kiuchumi.
Amesisitiza kuwa serikali inajitahidi kuhakikisha kila mwananchi anapata maji safi na salama kwa maendeleo ya jamii.
Kwa upande wao Madiwani wa kata za Ngumbo na Liwundi wameeleza furaha yao kwa serikali baada ya miradi ya maji kufanikisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Mradi wa Maji wa Ngumbo Group awamu ya pili unatekelezwa na Mkandarasi Mzawa, NIPO AFRICA ENGINEERING COMPANY LIMITED kutoka Dodoma, kwa gharama ya zaidi ya Shilingi bilioni 2.
Mradi huu unafadhiliwa na Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF), Serikali Kuu (GoT), na P4R. Utekelezaji ulianza Novemba Mosi 2023, na awali ulitarajiwa kukamilika Aprili 30, 2024, lakini kutokana na changamoto mbalimbali, muda wa utekelezaji umeongezwa hadi Juni 30, 2025.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.