MBUNGE wa Jimbo la Mbinga mjini mkoani Ruvuma Jonas Mbunda,amewataka wananchi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la orodha la wapiga kura ili wapate haki ya kushiriki na kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika hivi karibuni nchini kote.
Mbunda,amesema hayo baada ya kujiandikisha katika Daftari la wapiga kura katika kituo cha Ruhuwiko B kata ya Ruhuwiko Mbinga mjini.
Alisema,zoezi la kujiandikisha katika Daftari la Wapiga kura lina umuhimu mkubwa kwa Watanzania kwa kuwa linatoa nafasi kwa kila Mtu mwenye sifa kuchagua kiongozi anayemtaka katika mtaa,kitongoji na kijiji.
Alisema,viongozi hao ni muhimu kwa kuwa wanatakiwa kwenda kufanya kazi kwa kushirikiana na wananchi ili kuwaleta maendeleo na kusimamia miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo yao.
Mbunda alieleza kuwa,uchaguzi wa Serikali za mitaa ni daraja ambalo litawasaidia Watanzania kushiriki vyema katika uchaguzi Mkuu wa Madiwani,Wabunge na Rais utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka 2025.
“Wito wangu kwa wananchi wa Jimbo la Mbinga mjini kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kujiandikisha ili waweze kupata nafasi ya kikatiba ya kuchagua viongozi tunaowataka katika maeneo yetu”alisema Mbunda.
Aidha, amewaomba wananchi wa Jimbo la Mbinga Mjini kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili kuchagua viongozi wanaofaa ambao watawaletea maendeleo na kuepuka kuchagua viongozi kwa misingi ya ukabila na udini.
Kwa upande wake Afisa Mwandikishaji wa kituo cha Ruhuwiko B Witness Makoy alisema,zoezi hilo linaendelea vizuri huku idadi kubwa ya wananchi wakiendelea kujitokeza kujiandikisha.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.